Na Boaz Mazigo - Geita RS
Katika kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe.Martine Shigela amekutana na kufanya kikao cha kimkakati na wataalam mbalimbali wa Halmashauri za Mkoa wa Geita kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kuboresha lishe na kuondoa Udumavu kwa watoto hasa wenye umri chini ya miaka 5, jambo ambalo limekuwa likichangia hata ufaulu duni wa wanafunzi kutokana na historia ya makuzi na vyakula walivyokuwa wakivitumia.
Kikao hicho kiliketi Desemba 8, 2023 siku moja kabla ya siku ya maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara kilichofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Nyankumbu iliyopo mjini Geita ambapo pamoja na mjadala uliofanyika, iliazimiwa kuwa suala la Lishe liwe ni Agenda ya kudumu kwenye vikao mbalimbali ili kuendelea kupata matokeo chanya.
Akizungumza kabla na baada ya kuhitimisha kikao kazi hicho, mkuu wa mkoa wa Geita Mhe.Martine Shigela alisema ni muhimu kuzingatia maazimio ya kikao hicho ikiwemo kila Halmashauri kuhakikisha fedha iliyotengwa kwenye bajeti kwa ajili ya lishe inatolewa yote lakini pia kuhakikisha zinatenga shilingi 1,000 kwa kila mtoto kwenye eneo la lishe.
"kwanza niwapongeze viongozi wa Halmashauri kwa kuwezesha wataalam hawa mbalimbali kufika kwenye kikao hiku muhimu. Suala la lishe si la idara ya afya pekee, tushirikiane sote kwa pamoja ili tuweze kufanikiwa. Maazimio tuliyoweka, viongozi ngazi ya wilaya na Halmashauri muyasimamie", alisema RC Shigela
Vilevile RC Shigela alisema, ni vyema watumishi wa Umma kuwa na umoja na mshikamano na kwamba kwa kufanya hivyo ni rahisi kupata mafanikio, kisha kuhitimisha kwa kuzindua kitabu cha Mpango wa Utekelezaji wa Mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma ya Chakula na Lishe kwa Wanafunzi wa Elimumsingi.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Nicholas Kasendamila alisema," ninakupongeza sana RC Shigela kwa uongozi wako, unaipenda kazi yako. Na muhimu kwa watumishi ni kwamba, ili tufanikiwe ni muhimu tupendane, tuthaminiane, tujaliane na tuheshimiane, tusitegesheane. Pia, nisisitize juu ya uadilifu kwani unaleta mafanikio hadi kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya CCM"
Kwa upande mwingine, kaimu katibu tawala mkoa Dkt.Elfas Msenya alisema atahakikisha maelekezo na maazimio yanawafikia wahusika na yanatekelezwa.
Mganga mkuu wa mkoa Dkt. Omari Sukari alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wataalam wa afya kutoa elimu kwa wananchi kuchukua tahadhari kufuatia ugonjwa wa kipindupindu ulioripotiwa mkoa jirani na kwamba endapo wataona mtu mwenye dalili zozote zinazoashiria ugonjwa huo, basi hatua zichukuliwa kwa wakati na endapo watapatikana wagonjwa watibiwe kule walipo na wasihamishwe kwani kwa kufanya hivyo kutapelekea kusambaza ugonjwa na kwamba atasimamia watumishi wa afya kuenenda kwa weredi
Dkt. Sukari aliongeza kuwa, matarajio ya Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kutoa huduma bora kwa wananchi, hivyo mtumishi mzembe hatovumiliwa na pia aliwakumbusha watumishi wa sekta ya afya kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii wakizingatia maadili ili kuepusha taharuki wanaporusha mambo yao binafsi mtandaoni.
Kikaokazi hicho cha kimkakati kiha viongozi wa CCM Mkoa na wilaya, Kamati ya Usalama Mkoa, Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Geita, Wenyeviti wa Halmashauri zote za Geita, Makatibu Tawala Wilaya Wote, Wakurugenzi Watendaji Halmashauri zote za Geita, Wenyeviti kamati za kudumu za huduma za jamii za Halmashauri, timu ya afya mkoa, waweka hazina, maafisa utumishi, maafisa mipango, maafisa elimu, waganga wakuu, waratibu elimu kata, watendaji wa kata, maafisa lishe, maafisa Tarawa, viongozi wa vyama rafiki vya siasa pamoja na wadau wa Maendeleo
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa