Jubilei ya Miaka 50 Yaleta Faraja kwa Shule ya Msingi Kalangalala
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, ameendesha harambee wakati wa kuadhimisha Jubilei ya miaka hamsini (50) tangu kunzishwa kwa Shule ya Msingi Kalangalala iliyopo Mjini Geita iliyofanyika katika eneo la shule hiyo tarehe 19.11.2018 ambapo zaidi ya Shilingi Milioni Hamsini na Nane (Tshs. 58,000,000/=) zimetolewa ikiwa ni jumla ya fedha taslimu na ahadi katika kuhakikisha shule hiyo kongwe inafanyiwa ukarabati.
Mhandisi Gabriel ambaye alikuwa ni mgeni rasmi wa shule hiyo, ameeleza juu ya kutofurahia mwonekano wa shule hiyo iliyo usoni mwa barabara lakini pia iliyopo kwenye mkoa wenye dhahabu.
Amesema, “tunataka Geita inayomelemeta, lini? Ni sasa. Haiwezekani shule hii iko Mjini na majengo yake yachakae namna hii, tutafanya kitu. Lazima pia tuboreshe mazingira ya walimu kufanya kazi kama kuwa na nyumba bora za kuishi maeneo yote yenye changamoto”. Pia, Mgeni ramsi ameupongeza uongozi wa shule kwa kuwa wabunifu na kuja na wazo la kufanya ukarabati wa shule, vilevile kwa namna ambavyo wamekuwa na jitihada katika kuwafundisha wanafunzi shuleni hapo kisha akaahidi kuleta milioni hamsini (tshs.50,000,000/=), na kompyuta kwa ajili ya chumba cha TEHAMA zilizowezesha kufikia jumla kuu ya kiasi hicho cha fedha kilichochangwa.
Baada ya harambee hiyo, Mhandisi Gabriel aliagiza kuundwa kwa kamati maalumu ya ukarabati huku akisisitiza kuanza kwa ukarabati huo kuanzia mapema wiki ijayo.
Kwa kutambua umuhimu na nafasi ya Chama Tawala yaani CCM katika utekelezaji wa ilani yake, Kamati ya shule ikauomba uongozi wa chama hicho kukutana nao ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza ili kutekeleza ilani ya CCM vizuri.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita, Mhandisi Modest Apolinary aliwapongeza walimu huku akiwaambia tayari ameidhinisha fedha za kuanza uboreshaji wa bustani za shule mbili za Kalangalala na Nyanza na hivyo kwa mwaka ujao, Halmashauri itajenga shule mbili za kisasa za msingi ili kupunguza msongamano katika shule za Nyanza na Kalangalala kwa lengo la kuwapatia wanafunzi elimu iliyo bora.
Akisoma taarifa ya shule, mwalimu mkuu wa shule hiyo Mwl. Regina C. Ketau amesema, shule hiyo ilianzishwa rasmi tarehe 05.11.1968 kama shule ya Serikali na kwamba kabla ya hapo ilikuwa ikisimamiwa na Jumuiya ya Wazazi (TAPA). Pia shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,809 wa elimu ya msingi wavulana wakiwa 807 na wasichana wakiwa 831 na kwa upande wa elimu ya awali wavulana 79, wasichana 88.
Mwl. Ketau alieleza changamoto zinazoikabili shule hiyo zikiwemo uchakavu wa majengo, upungufu wa vyumba vya madarasa kwakuwa vilivyopo ni 40 lakini vinavyohitajika ni 13, hivyo pungufu kuwa vyumba 27. Ukosefu wa chumba cha TEHAMA, Umeme na uzio jambo ambalo mgeni rasmi aliahidi kuyapatia masuala yote ufumbuzi ikiwemo kuwekwa umeme kwa vyumba vyote.
Awali, walimu walimtembeza mgeni rasmi ili ajionee madarasa yanayozungumza, yaani madarasa ambayo hata mwalimu akiwa hajaingia darasani basi wanafunzi huweza kujisomea wenyewe yaani Mahili ambapo alijionea mahili za mawasiliano, kuhesabu, huduma ya kwanza, michezo na afya, kuandika n.k
Miongoni mwa waliohudhuria na kuchangia harambee hiyo ni pamoja na Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya, Viongozi wa CCM, Idara ya Elimu Sekretarieti ya Mkoa, Viongozi wa Dini, Uongozi wa CWT, Uongozi wa Makoye Hospital, Redio ya Strom FM Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Kata ya Kalangalala, Uongozi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Walimu wa Shule ya Msingi Kalangalala, Diwani wa Kalangalala, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Kampuni ya Simu ya Tigo bila kusahau Kamati ya Shule.
Mwisho, sherehe hiyo ilimalizika kwa kukata keki kama ishara ya kumbukumbu ya kuanzishwa shule hiyo na kutoa vyeti mbalimbali kwa waalimu na burudani mbalimbali kutoka kwa wanafunzi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa