Katika kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Shirika lisilo la kiserikali la Plan International limetoa vifaa vya michezo na kujifunzia kwa wanafunzi wa shule za awali na msingi katika wilaya za Geita, Chato na Nyang’hwale vitakavyowanufaisha zaidi ya wanafunzi elfu mbili waishio katika mazingira magumu.
Msaada huo umetolewa machi 29, 2019 katika ofisi za Plan International Geita kama ishara ya kuzindua usambazaji wa vifaa hivyo na kukabidhiwa mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Josephat Maganga ambapo amewashukuru wadau hao kwa namna wanavyotambua jitihada za serikali kwa kuziunga mkono si tu kwenye sekta ya elimu bali pia kwenye sekta nyinginezo.
“nawapongeza sana shirika la Plan International kwa mchango wenu mkubwa mnaoutoa na mnaoendelea kuutoa tukitambua kazi kubwa inayofanywa na Mhe. Rais Magufuli, lakini pia tutambue yakuwa, serikali kwa kuwajali wananchi wake imeleta elimu bila malipo ambayo nayo imechangia ongezeko la wanafunzi ambao awali walishindwa kuhudhuria masomo kutokana michango mbalimbali” amesema Maganga.
Hakuishia hapo, Maganga ameeleza kuwa, mkoa wa geita kwa mwaka 2018/2019 umepokea zaidi ya Shilingi Bilioni 4.8 ikiwa ni fedha za ujenzi wa miundombinu mipya ya shule za msingi na sekondari lakini pia ukamilishaji wa miundombinu hiyo iliyokuwa ikijengwa akisema, “haijawahi kutokea” kwakweli hii ni hatua kubwa na ya mafanikio kwa serikali ya Tanzania.
Maganga amewataka watendaji wa serikali kuhakikisha vifaa tolewa kwa wanafunzi na shule vinawafikia walengwa na kufanya kazi kama ilivyokusudiwa huku akiwasisitiza wanafunzi waliohudhuria uzinduzi huo, kuhakikisha wanavitunza na kuvitumia vyema vifaa hivyo akiwaonya wazazi kutobadili matumizi ya vifaa hivyo, kisha akatoa wito kwa wadau wote ndani ya mkoa wenye nia njema kujitokeza kuunga mkono sekta ya elimu kwakuwa bado uhitaji ni mkubwa na kumaliza kwa kuzindua zoezi la usambazaji vifaa hivyo na kugawa baadhi kwa wanafunzi waliokuwepo.
Meneja Mradi wa Tokomeza Ajira kwa Watoto kutoka Shirika la Plan International Emma Mashobe katika taarifa ya mradi amesema, shirika limetoa vifaa hivyo vya michezo na kufundishia kwa shule za awali, bendi kwa shule za msingi pamoja na mahitaji mbalimbali ya wanafunzi kama vile mabegi, sare za shule, madaftari, kalamu, mikebe na rula, vifaa ambavyo ni muhimu kuwasaidia waendelee kuwepo mashuleni. Vifaa vya michezo na kufundishia ni pamoja na mbao, mipira na kamba za kuruka.
Mashobe amesema, vifaa vyote tolewa vina thamani ya zaidi ya shilingi milioni mia mbili kumi na moja na vitawanufaisha watoto zaidi ya elfu mbili katika kata 17 ndani ya wilaya za Geita, Chato na Nyang’hwale huku akilishukuru Shirika la Maendeleo la Ufaransa AFD kwa ufadhili wa mradi huo wakiamini, uwepo wa mradi huo utapunguza ajira hatarishi kwa watoto kwa kuwapa chachu wanafunzi wasome na ni utekelezaji wa shughuli kuu za shirika za maendeleo ya jamii kwa kumuweka mtoto kama kiini au moyo.
Kipekee, Mashobe akaiomba serikali kuimarisha bajeti kwa maendeleo na ustawi wa jamii, kuboresha idara ya kazi katika kuhimiza ukaguzi wa sehemu za kazi kuona kwamba migodi na sehemu nyingine za kazi zinakaguliwa.
Naye Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Elimu Mkoa wa Geita Kaitira Mafwimbo, amewapongeza Plan International na kumuahidi mwakilishi wa mgeni rasmi kuwa sekretarieti itasimamia na kuhakikisha vifaa vinawafikia walengwa na vonatunzwa.
Mwanafunzi wa darasa la pili mwenye ulemavu wa viungo Restuta Sayenda kutoka shule ya msingi Buselesele wilayani Chato ameshukuru kwa msaada uliotolewa akiamini utamsaidia yeye na wenzake kwa ujumla na kwamba vifaa hivyo vitatumiwa ipasavyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa