Zaidi ya wachimbaji wadogo wa madini 400 kutoka halmashauri zote za mkoa wa geita wamejengewa uwezo juu ya kurasimisha uchimbaji wao, kuzingatia kanuni na sheria za madini, ulipaji kodi, kupitia jukwaa la mtaji wa maendeleo kwa muda wa siku 3 lililoandaliwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) wakishirikiana na Godtec lililofanyika katika ukumbi wa GEDECO halmashauri ya mji Geita tarehe 11.07.2019 kwa udhamini wa benki ya NMB.
Akifunga jukwaa hilo, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo ameipongeza Benki ya NMB ya kuendelea kuwashika mkono wachimbaji wadogo wa madini, kundi kubwa lakini lisiloaminika kwa taasisi nyingi za kifedha, huku akitoa wito kwa NMB, MKURABITA na wadau wengine kuendelea kuandaa majukwaa ya fursa katika mikoa mbalimbali nchini na kuwataka wachimbaji wadogo kutekeleza kwa vitendo yale waliyoyapata katika jukwaa hilo
Naibu Waziri Nyongo amesema, “nimekuja kuunga mkono wazo la urasimishaji na uendelezaji sekta ya uchimbaji mdogo ili kuongeza uzalishaji utakaoongeza pato binafsi. Niwapongeze MKURABITA, STAMICO na Kampuni binafsi ya Godtec kwa uratibu mzuri. Vilevile niwapongeze uongozi wa Benki ya NMB ambao mmekubali kufadhili, hii ni dalili tosha kwa utayari wa uongozi wa benki hii katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe.Rais Magufuli katika kuwezesha wananchi kiuchumi ili kila mmoja awe na mchango katika kujenga Tanzania ya viwanda”.
Naibu Waziri Nyongo anaamini kuwa, mafanikio ya jukwaa hili mkoani geita ni chachu ya kuwafikia wachimbaji wadogo maeneo mengine.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Nyongo amesema, serikali ina mkakati wa kuendelea kupitia leseni zote za utafiti hususan maeneo makubwa ili kubaini leseni zinazofanya kazi na wachimbaji kupewa rai kuwekeza katika maeneo mengine tofauti na madini kwani geita inazo fursa kemkem hivyo wasidanganyike na msemo kuwa “dhahabu ipo tu” wakati inaweza kuisha.
Mkuu wa mkoa wa geita mhandisi Robert Gabriel amesema anawahakikishia wananchi wote wanaostahili kulipwa fidia kutokana na madhara yaliyotokana na shughuli za mgodi wa GGM watalipwa na malalamiko yote yatashughulikiwa huku akiwatia moyo wanawake wachimbaji wadogo kuwa wanao uwezo wa kumiliki migodi hivyo wakati wao ni sasa na akitumia fursa hiyo kuialika wizara kushiriki katika maonesho ya pili ya teknolojia ya dhahabu yanayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 20 -29/09/2019.
Mhandisi Gabriel amewasilisha maombi kwa mgeni rasmi ikiwemo serikali kutoa maeneo yenye uhakika wa upatikanaji madini kwa wachimbaji wadogo na wananchi kuwa na vikundi rasmi vinavyotambulika na kuwezeshwa kwa kupewa mitambo ya kisasa kwa uzalishaji.
Naibu waziri wa maliasili na utalii Constantine Kanyasu yeye amewaeleza washiriki wa jukwaa hilo kuwa, ni muhimu kufuata taratibu wakiomba vibali pale wanapohitaji kuchimba katika maeneo ya hifadhi na kinyume cha kufanya hivyo wataitwa wavamizi ukizingatia sasa lipo jeshi USU kwa ulinzi wa lasilimali hifadhi.
Naye Mkurugenzi wa MKURABITA Dkt. Seraphia Mgembe amesema, anamshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuteua Mawaziri vijana na wachapakazi huku akimshukuru mgeni rasmi kwa kufika huku akiwashukuru pia wachimbaji wadogo wa geita kwa kuhamasika kwakuwa walipita kuhamasisha karibu katika kila kata 2 wilaya zote wanazojishughulisha na uchimbaji bila kusahau shukrani kwa mdhamini Benki ya NMB.
Dkt. Mgembe ameendelea kutoa elimu kuwa MKURABITA inashughulika pia na wachimbaji wadogo ili kuhakikisha wanamiliki ardhi, nyaraka mbalimbali zitakazowawezesha kukopesheka kuendeleza kazi zao, hivyo amewaasa wachimbaji kujifunza kutunza taarifa za shughuli zao ili wajue wamezalisha na kutumia kiasi gani.
Kwaniaba ya Benki ya NMB, Filbert Mponzi amesema, wao ni wadau wakubwa katika kuwahudumia wajasiliamali wadogo na wa kati, hivyo kila mwezi NMB hutoa zaidi ya Bilioni 40 kama mikopo kwa wajasiliamali na kwamba, jitihada za serikali ya awamu hii ya tano ndizo zimewapelekea kupata hamu ya kujishughulisha na wajasiliamali.
Mponzi ameendelea kusema kuwa, baada ya ufunguzi wa soko la dhahabu geita, waliona ni lazima waje na mpango wa kuwasaidia wachimbaji wadogo, hivyo wazo la MKURABITA pampja na Godtec limekuwa muhimu kwao hadi kuamua kuliteleza.
Taasisi nyingine zilizohusishwa kama watoa mada ni pamoja na TRA, Tume ya Madini, STAMICO, Busolwa Mining, MOMCO na GEREMA
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa