Katibu Tawala Mkoa wa Geita Ndugu. Mohamed Gombati amewaasa viongozi wa dini ambao ni wajumbe wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Geita kuhakikisha wanatumia busara na hekima walizojaliwa na Mwenyezi Mungu kuhamasisha Amani, upendo na mshikamano katika kipindi hiki ambapo Kampeni za wagombea wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hapo Novemba 2027 zimeanza.
Katibu Tawala Mkoa wa Geita ametoa kauli hiyo hini karibuni aliposhiriki kikao cha Kamati hiyo kujadili namna ya kutoa elimu kwa jamii juu ya kuwa watulivu, washikamane na kuwa na Amani kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Ndugu zangu viongozi wa dini napenda kutumia wasaa huu kuwaeleza kuwa tumieni nguvu zenu kuwashauri viongozi wa vyama vyote vya siasa pamoja na wanachama wao kutumia maneno ya hekima na lugha yenye staha wakati wa kampeni za Uchaguzi zilizoanza tarehe 20 Novemba 2024. Pia kila mmoja azingatie Sheria, Kanuni na taratibu za Uchaguzi ili Uchaguzi utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu uwe wa Amani.” Aliongeza Ndg. Mohamed Gombati.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita ameeleza kuwa Serikali ya Mkoa inaamini zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa litawaunganisha watu na sio kuleta mipasuko wala chuki baina ya kundi Fulani na kundi jingine. Kadhalika amewashauri viongozi wa dini kuwahamasisha wananchi kutumia fursa zilizopo katika Mkoa kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji madini na biashara ndogo ndogo ili wajikwamue kiuchumi na kupata maendeleo yao binafsi na jamii nzima.
Ndg. Mohamed Gombati pia ametoa rai kwa wakazi wote wa Mkoa wa Geita kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya tarehe 27 Novemba 2027 katika vituo walivyojiandikishia. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza kuwa siku hiyo itakuwa ni mapumziko ili wananchi wapate nafasi ya kuchagua viongozi watakaowaongoza katika maeneo yao.
Sheikh wa Mkoa wa Geita Sheikh. Yusuph Kabaju amesema kuwa wao kama wajumbe wa Kamati ya Amani ya Mkoa na viongozi wa dini wamejipanga kuzungumza na waumini wao ili kuwajenga weweze kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa Amani, utulivu na mshikamano mkubwa pasipo kuweka mbele maslahi ya vyama vyao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa