Mradi wa visima virefu 150 vya kilimo cha umwagiliaji vitakavyojengwa katika Halmashauri zote za Mkoa wa Geita utawanufaisha wakulima kwa kulima kilimo cha uhakika kupitia umwagiliaji kwa mwaka mzima.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika tarehe 16 Oktoba 2025 katika Kijiji cha Mwilima Kata ya Kanyala, Manispaa ya Geita, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya jambo la kukumbukwa na wakulima wa Mkoa wa Geita kwa sababu baada ya ujenzi wa visima hivyo watakuwa na uhakika wa kufanya shughuli za kilimo katika kipindi chote cha mwaka.
Mhe. Shigela amewasisitiza wakulima wa eneo la Kanyala na wilaya nyingine za Mkoa wa Geita kuutunza na kuuthamini mradi wa visima hivyo ambavyo vitawawezesha kuongeza uzalishaji wa mazao kupata kipato endelevu.
“Natoa wito kwa maafisa ugani wote kufanya utafiti wa udongo kwa ajili ya kuwaletea wananchi pembejeo zinazoendana na ardhi ya maeneo ya kilimo. Pia Serikali ya awamu ya sita imejipanga kuleta masoko na kujenga maghala sambamba na kuleta stakabadhi za mauzo hivyo mjipange kunufaika na mazuri yanayofanywa na Serikali yenu.” Aliongeza Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Kwa upande wake Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Geita Boniphace Mitika amesema kuwa mradi wa visima vya kilimo cha umwagiliaji vinatekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ambapo kwa awamu ya kwanza Mkoa wa Geita utatekeleza visima 36 katika vijiji 32 vyenye jumla ya ekari 1440 lenye zaidi ya wakulima 747.
Mhandisi Mitika ameongeza kuwa upatikanaji wa maji ya uhakika utaongeza uzalishaji wa mazao kwa kiwango kikubwa na kumpatia faida mkulima mdogo Pamoja na upatikanaji wa chakula cha kutosha kuanzia ngazi ya kaya hadi Taifa na kuwainua wakulima wadogo n awa kati kiuchumi.
Mradi wa uchimbaji visima virefu vya kilimo cha umwagiliaji umeibuliwa kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao kwa wakulima wadogo kupitia kilimo cha umwagiliaji. Mradi huu unasimamiwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wenye thamani ya Shilingi Bilioni 37.34
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa