Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa amebainisha kuwa maendeleo ya Nchi yameletwa na juhudi zinazofanywa na walimu katika kuhakikisha wanawajengea uwezo watu katika taaluma na fani mbalimbali zinazowapa ujuzi kwenye maeneo tofauti.
Mhe. Kassim Majaliwa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na maelfu ya walimu wa Shule za Msingi na Sekondari kutoka katika Halmashauri zote za Mkoa wa Geita waliohudhuria Maadhimisho ya siku ya Mwalimu Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Ushirombo Wilayani Bukombe tarehe 03 Oktoba 2025.
Mhe. Waziri Mkuu amefafanua kuwa kupitia juhudi na ubunifu wa walimu, watoto na vijana wa kitanzania wanajengewa maarifa, stadi za kazi na maadili ya kizalendo yanayowawezesha kuwa wajuzi katika kada mbalimbali zikiwemo udaktari, uhandisi, sheria na nyinginezo ambazo ndizo nguvu kazi zinazotegemewa katika jamii.
Mhe. Kassim Majaliwa ameongeza kuwa katika kutambua umuhimu wa elimu Nchini, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya kada ya elimu kwa kuajiri walimu wapya kila mwaka, kupandisha madaraja na kutoa fursa ya mafunzo mbalimbali kwa walimu.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amesema kuwa mwalimu ni binadamu pekee ambaye hutoa mwelekeo bora wa mtu katika maisha yake. Pia taaluma ya ualimu ndiyo inayomfanya mtu kuwa bora, raia mwema, mtumishi bora kuliko hata mwalimu mwenyewe hivyo kila mmoja aliyefanikiwa anatakiwa atambue kwamba kazi nzuri iliyofanywa na walimu ndiyo iliyomfikisha kwenye hatua hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Caroline Nombo ametoa pongezi kwa walimu wote wanaoendelea kutoa nguvu kazi zao, juhudi na maarifa katika kuhakikisha Taifa linapata wasomi wa kutosha.
Prof. Nombo ameongeza kuwa Serikali imeendelea kufanya shughuli mbalimbali zinazowezesha walimu kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya, mojawapo ikiwa ni kushirikiana na wadau ambao ni Mtandao wa Elimu Tanzania ambao wameandaa programu ya taaluma ya uongozi katika ufundishaji ambayo itafanywa kwa lengo la kuimarisha mbinu za ufundishaji, kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa walimu na kuongeza motisha ili kuboresha elimu Nchini.
Akitoa shukrani kwa Serikali ya awamu ya sita kwa niaba ya wananchi wa Geita, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ametoa pongezi kwa Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali mashuleni, kuwalipa walimu fedha za malimbikizo na kutoa fedha za elimu bila malipo ambazo zinawawezesha wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu kupata elimu bila tatizo.
Akisoma risala ya walimu, Katibu wa Chama cha Walimu Mkoa wa Geita Mwl. Pauline Ntinde ameeleza kuwa Maadhimisho ya siku ya walimu yalianza mwaka 2019 kwa lengo la kutambua na mchango wa walimu katika kujitolea kwao katika jukumu muhimu la kukuza na kuendeleza vipaji vya wanafunzi. Maadhimisho ya siku hiyo kwa mwaka 2025 yaliongozwa na kauli mbiu isemayo “ Walimu wetu, Fahari yetu”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa