Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ametoa wito kwa wakandarasi wote waliofanikiwa kusaini mikataba minne ya ujenzi wa miradi ya maji yenye thamani ya shilingi Bilioni 3.6 za Kitanzania ambayo itatekelezwa kwenye vijiji 12 katika Wilaya za Chato, Geita na Mbogwe.
Mhe. Shigela ametoa kauli hiyo hivi karibuni alipokuwa anashuhudia zoezi la utiaji Saini wa mikataba hiyo baina ya Wakandarasi watakaofanya kazi hiyo na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA). Hafla ambayo ilifanyika katika ukumbi mdogo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Mkuu wa Mkoa wa Geita ametumia nafasi hiyo kuwapongeza wataalam wa RUWASA kwa kuhakikisha wanaifanyia kazi maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumtua mama ndoo kichwani, na kuongeza kuwa baada ya kukamilika kwa miradi hiyo Mkoa wa Geita utafikisha asilimia 86% ya utoaji huduma ya maji.
“Miradi hii itakapokamilika kwa wakati uliokusudiwa utawawezesha wananchi kunufaika nayo na kuondokana na kero ya kufuata maji katika vijiji Jirani mbali na makazi yao na kuufanya Mkoa wa Geita kuondokana na tatizo la ukosefu wa maji safi na salama.” Aliongeza Mhe. Shigela.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini( RUWASA) Mkoa wa Geita, Mhandisi Jabiri Kayilla ameeleza kuwa miradi hiyo yam aji inatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji vijijini kwa asilimia nne, ambapo kwa sasa hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya vijijini ni zaidi ya asilimia 70% na baada ya utekelezaji wa miradi hiyo kukamilika Mwezi Aprili 2026 hali ya upatikanaji maji itaongezeka na kufikia asilimia 86%.
Miradi minne ya maji itakayotekelezwa katika vijiji vya Lwezera, Ikina, Bugogo, Ihega, Nyarugusu, Rumasa, Mabila, Ngemo, Bwendamwizo, Ilolangulu, Buningozi na Mpakali itatoa huduma kwa wananchi wapatao 27,000 wa maeneo hayo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa