Mchango wa Sekta ya Madini katika pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 6.8 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 10 mwaka 2024 huku mchango wa wachimbaji wadogo na mapato yote ya sekta ya madini ukiongezeka kutoka asilimia 20 mwaka 2020 hadi asilimia 40 mwaka 2024.
Takwimu hizo zimetolewa na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko alipokuwa akizungumza na hadhara ya wananchi wa Mkoa wa Geita wakati wa ufungaji rasmi wa Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini 2025.
Dkt. Biteko ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na jitihada za Serikali kuongeza ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya Madini ikiwa ni Pamoja na shughuli zote za mnyororo mzima wa thamani ya Madini Nchini, ambapo kwa Mkoa wa Geita pekee wachimbaji wadogo wamezalisha kilo 22,014.61 zenye thamani ya shilingi trilioni 3.43 na Serikali kukusanya mapato ya shilingi Bilioni 2.5 katika kipindi cha mwaka 2021/22 hadi 2024/25.
“Natumia fursa hii kuwapongeza wachimbaji wadogo,kati, wakubwa na Wizara ya Madini kwa mafanikio hayo yaliyowezesha kuinua pato la Taifa. Natoa wito kwenu kuendelea kubuni teknolojia za juu zaidi na kuongeza uwezeshwaji wa watanzania kuongeza thamani ya Madini wanayozalisha, mazingira hayo yataongeza upatikanaji wa fedha za kigeni Pamoja na kuwapatia watanzania kuongeza thamani ya Madini wanayozalisha.” Aliongeza Dkt. Biteko.
Naibu Waziri Mkuu amewahakikishia wadau wote wa sekta ya Madini kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya Madini ikiwemo kufikisha huduma ya umeme katika maeneo yote yanayohitaji huduma hiyo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Ndg. Msafiri Mbibo amesema kuwa Wizara ya Madini itaenbdelea kusimamia sheria na taratibu zote ili kuifanya sekta hiyo kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa. Pia ameeleza namna Maonesho ya Teknolojia ya Madini yalivyokuwa chachu hususan kwa wachimbaji wadogo kwa kuwaongezea elimu kuhusu uchimbaji hatarishi na matumizi ya zebaki.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kutolewa kwa leseni 9,000 kwa wachimbaji wadogo wakiwemo wa pori la Kigosi ikiwa ni hatua ya Serikali katika kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata maeneo yatakayowapa fursa ya kujikwamua kiuchumi.
Maonesho ya Teknolojia ya Madini 2025 yamebebwa na Kauli Mbiu isemayo ‘Ukuaji wa Sekta ya Madini ni Matokeo ya Matumizi ya Teknolojia Sahihi na Uongozi Bora, Shiriki Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025.’ Jumla ya washiriki 930 wakiwemo washiriki kutoka nje ya Nchi wameshiriki ikilinganishwa na washiriki 600 waliokuwepo mwaka 2024.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa