Hali ya Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI katika Mkoa wa Geita imeshuka kwa asilimia 4.9% ikiwa yamepungua kwa asilimia 0.1% kutoka wastani wa mwaka 2016/17 ambapo maambukizi yalikuwa 5.0%
Takwimu hizo zimebainishwa na Mratibu wa UKIMWI Mkoa wa Geita Dkt. Yohane Kihaga hivi karibuni wakati wa Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika kimkoa katika kata ya Bukwimba Wilaya ya Nyang’hwale.
Dkt. Kihaga ameeleza kuwa Mkoa wa Geita unakadiriwa kuwa na watu 95,100 wanaoishi na virusi vya UKIMWI kati ya watu hao asilimia 73.1 wanatambua hali ya maambukizi ya VVU, na asilimia 98.4 ya hao wanatambua hali zao na wanatumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI, huku asilimia 98.8 wakiwa tayari wamefubaza VVU.
Mratibu wa UKIMWI Mkoa wa Geita amebainisha mazingira yanayochochea mwendelezo wa maambukizi ya Virusi vya UKIMWI katika Mkoa wake ni pamoja na hekaheka za mapambano ya maisha ikijumuisha maeneo ya uchimbaji mdogo wa dhahabu, uvuvi, minada, maegesho makubwa ya malori, vilabu vya pombe za asili na ujenzi wa miradi mikubwa kama Bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda.
Dkt. Kihaga amebainisha kuwa Mkoa wa Geita umelenga kushirikiana na wadau kuhakikisha wanapambana na tatizo la Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa kuendelea kutoa elimu juu ya tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya VVU kwa kutumia njia rafiki watakazozibuni pamoja na kufanya upimaji wa VVU kwa kuwafuata watu kwenye maeneo maalum wanayoishi au kufanyia shughuli.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Hashim Komba ametoa rai kwa vijana na wanaume kujenga utamaduni wa kupima afya zao ili kujitambua na sio kutegemea majibu yanayopatikana baada ya wake zao kupimwa kipindi cha ujauzito.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita ASCP Safia Jongo ametoa wito kwa jamii kuhakikisha wanawalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili pamoja na kuwakinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ili waweze kutimiza malengo yao katika maisha.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, Ndg. Ponsian Magezi ametoa wito kwa Serikali kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili watu wanaoishi na maambukizi ya VVU wasinyanyapaliwe wala kutengwa katika jamii.
Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuikumbusha jamii juu ya uwepo wa janga la UKIMWI na athari zake ili kuweza kuchukua tahadhari za kujilinda. Kwa mwaka 2024 Maadhimisho hayo yameongozwa na Kauli Mbiu isemayo"CHAGUA NJIA SAHIHI, TOKOMEZA UKIMWI".
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa