Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa amewaasa wadau pamoja na wananchi wote wa Mkoa wa Geita kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha sekta ya Madini kwa maendeleo ya Taifa.
Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na hadhara ya wananchi waliojitokeza kwa wingi kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa Maonesho ya nane ya Teknolojia ya Madini tarehe 22 Septemba 2025 katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Bombambili Geita Mjini.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameeleza kuwa sekta ya Madini ni injini muhimu ya maendeleo ya Taifa na inaweza kuleta manufaa makubwa kwa kizazi cha sasa na kijacho iwapo itaendelezwa kwa weledi, uwazi na uadilifu.
“Leo hii Mkoa wa Geita unapata heshima kuwa mkoa unaoongoza kwa uzalishaji wa dhahabu Nchini,hii imewavutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza na matokeo yake mji unazidi kukua kwa kasi na maisha ya wananchi yameendelea kuboreka na Serikali inaahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kuendeleza Sekta ya Madini”. Aliongeza Mhe. Waziri Mkuu.
Akizungumza katika ufunguzi huo Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ameeleza kuwa katika kutekeleza agizo la viongozi wakuu waliofika katika Maonesho ya miaka ya nyuma tangu yalipoanzishwa ambapo waliagiza kujengwa kwa miundombinu ya kudumu, mwaka huu majengo tisa ya kudumu yamejengwa kupitia misingi ya watu wanaopendana, kuheshimiana na kuthaminiana hatimaye kupelekea kufanikisha ujenzi wa awali wa miundombinu ya kudumu.
Mhe. Shigela ameongeza kuwa Mkoa wa Geita umefanikiwa kuzalisha kilo 22,000 za madini ya dhahabu zenye thamani ya shilingi trilioni 3.4 kutoka kwa wachimbaji wadogo ndani ya kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025 na Serikali kupata mrabaha wa Shilingi Bilioni 235.5 Kadhalika ndani ya kipindi cha uongozi wa Serikali ya awamu ya sita leseni za wachimbaji wadogo zimefikia 9000 mwaka 2025 kutoka leseni 900 kwa mwaka 2021.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa