Wafanyabiashara wadogowadogo Mkoani Geita wamepatiwa elimu ya fursa zinazotolewa na serikali kupitia Benki ya NMB.
Akizungumza katika kongamano la wafanyabiashara wadogowadogo Septemba 19 katika ukumbi wa Mkapa Bombambili Geita mjini, Mgeni rasmi Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Geita Dkt.Elfasi Msenya amesema lengo kuu ni kuhakikisha wafanyabiashara wadogo wadogo wanapata elimu ya kuzitambua fursa zinazotolewa na serikali ambapo wafanyabiashara watanufaika na mikopo ya zaidi ya shilingi milioni 80 zinazotolewa na serikali kupitia benki ya NMB.
Dkt.Msenya amesisitiza kuwa ni jukumu la maafisa maendeleo ya jamii kufanyia kazi maoni, changamoto na ushauri unaotolewa na wafanyabiashara wadogowadogo ili kuhakikisha mazingira ya biashara yanakuwa rafiki.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Geita Bi. Martha Kaloso ametoa taarifa hiyo katika kongamano hilo amesema kuwa Mkoa wa Geita umefanikiwa kusajili jumla ya wajasiriamali 1,142 katika mfumo wa urasimishaji kwa ajili ya utoaji wa vitambulisho na utoaji wa mikopo ya asilimia saba iliyotengwa na Serikali kuu tangu zoezi hilo lilipoanza hadi Septemba 2025.
Bi. Martha Kaloso ameongeza kuwa kati ya wajasiriamali hao waliopata mkopo mpaka sasa ni 54 kupitia mkopo wa asilimia saba unaotolewa na Serikali kuu kupitia Benki ya NMB ambao wamepatiwa jumla ya Shilingi Milioni 124. Miongoni mwa walionufaika ni pamoja na mama lishe waliopata shilingi milioni 6.6, machinga shilingi milioni 105 na wajasiriamali wengine wadogo wakipatiwa shilingi milioni 133.
Kwa upande wake Meneja wa NMB Geita Bw.Daniel Lawia ametoa elimu kwa wafanyabiashara wadogowadogo juu ya namna ya kufanya pindi wanapofuatilia mikopo na amewaomba wafanyabiashara kuepukana na udanganyifu wa maeneo yao ya biashara pindi wanapofuatilia mikopo.
Mwakilishi wa Shirika la SIDO Mhandisi Cosmas Kinasa limewahimiza wafanyabiashara wadogo kupata ushauri wa kitaalam kuhusu namna bora ya kuendesha biashara.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa