Ikiwa ni mwendelezo wa Wiki ya Utumishi wa Umma nchini, Katibu Tawala Mkoa wa Geita Denis Bandisa amekutana na kuzungumza na watumishi wa umma ngazi ya sekretarieti ya mkoa akisikiliza changamoto zinazowakumba, ikiwa ni mojawapo ya programu zilizoandaliwa katika maadhimisho ya wiki hii muhimu kwa watumishi, kikao kilichofanyika Juni 18, 2019 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa geita.
Akielezea umuhimu wa wiki ya utumishi wa umma, Bandisa amewashukuru watumishi hao kwa namna ambavyo wameonesha ushirikiano kwa kipindi chote ambacho ameendelea kutumikia katika nafasi hiyo, huku akiwataka kuendelea kushikamana, kushirikiana, kufanya kazi kama wamoja pamoja na kuwa na mahusiano mazuri baina ya watumishi katika kutekeleza majukumu ya kiutumishi.
“ninashukuru sana kwa ushirikiano wenu, utumishi bila kupendana na kushirikiana hauwezi kusogea. Nimewaita tuongee changamoto, tujadiliane, tutatue, ili twende mbele na hivi ndivyo tunavyoadhimisha wiki hii lakini pia tuongeze juhudi”, alisema Bandisa
Bandisa aliendelea kusema kuwa, katika wiki hii atazunguka na kuongea na watumishi wa umma walioko kila halmashauri ndani ya mkoa huu kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili ili kuweka mazingira rafiki ya kufanyia kazi, kisha kupokea maoni na changamoto za watumishi hao.
Akiongea kabla ya kumkaribisha mwenyekiti wa kikao hicho, katibu tawala msaidizi, Utawala na Rasilimali Watu Herman Matemu amesema, pamoja na kikao hicho, wiki hii kutakua na programu mbalimbali ikiwemo mafunzo ya ujazaji wa fomu za Opras katika kuboresha utendaji kazi wa watumishi.
Deborah Zella, David Makabila, Masoud Biteyamanga, Abdallah Mfaume, dkt Japhet Siemeo na Felix Mabula ni baadhi ya watumishi waliotoa maoni na michango mbalimbali katika kikao hicho wakiwakilisha watumishi wengine huku wengi wao wakigusia juu ya maslahi ya watumishi kufanyiwa kazi kwa wakati.
Halikadhalika katika kikao hicho, Mkuu wa kitengo cha TEHAMA ofisi ya mkuu wa mkoa wa geita Lazarus Moshi akatumia nafasi hiyo kuwashauri watumishi kuendelea kuwa na matumizi bora ya vifaa vya TEHAMA kwa kulinda siri za ofisi huku akiahidi kuboresha mawasiliano ya kieletroniki ndani ya ofisi hiyo.
Kikao kilihitimishwa kwa kuwaacha watumishi katika ari mpya ya kufanya kazi, huku wakiahidi kuendeleza Juhudi, mshikano, ushirikiano na kusaidiana ili kwa pamoja kuwatumikia wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa