Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amezindua kampeni ya usafi wa mazingira ya mtaa kwa mtaa itakayodumu mwezi mzima ikihamasisha usafi kuwa endelevu katika kuhakikisha Mji wa Geita ambao umekuwa ndoto ya wana Geita kuwa Manispaa basi ufikie hatua hiyo kwa kuzingatia vigezo vyote ikiwemo usafi wa mji.
RC Gabriel amewaongoza wananchi wa Mtaa wa Shilabela, Kata ya Buhalahala kufanya usafi katika maeneo yote ya mtaa huo likiwemo eneo la soko tarehe 03.11.2018 ambapo mamia ya wakazi na wafanyabiashara wa eneo hilo wamejitokeza kuunga mkono juhudi za RC Gabriel akiwa mbele akiongoza zoezi hilo, huku akiwashukuru wananchi waliojitokeza wakiwa na vifaa mbalimbali vya usafi bega kwa bega pamoja naye.
Akiongea na wananchi baada ya zoezi hilo la usafi, RC Gabriel amesema, “tumezindua kampeni hii ya usafi, ni endelevu na ya mtaa kwa mtaa, tunajenga Geita mpya ili mji wetu ufanane na dhahabu kwakuwa wengine husema pamba ni dhahabu nyeupe, korosho ni dhahabu ya kijani ila Geita tunasema Dhahabu tunayo orijino yaani halisi” hivyo kuwahamasisha wananchi hao kuyatunza mazingira.
RC Gabriel ametoa onyo kwa watendaji wasiosimamia vyema matokeo ya fedha zinazochangishwa kwa wananchi kusafisha mazingira akisema ni lazima fedha inayokusanywa kwa ajili ya usafi zioneshe matokeo yaani maeneo yawe safi. Vilevile amekemea tabia ya baadhi ya watendaji kutokusoma taarifa za mapato na matumizi jambo ambalo huleta mashaka kwa wananchi. Wanaume pia wakaonywa kupitia hadhara hiyo kuhusu kuacha tabia za kuwanyanyasa kwa kuwapiga wake zao, huku waganga wa jadi wapiga ramli chonganishi wakifikishiwa ujumbe kuwa hawana nafasi Geita.
Hakuishia hapo tu, bali pia RC Gabriel ameitaka kampuni inayohusika na usafi Mjini Geita iitwayo Workers General Supply kuhakikisha maeneo yanakuwa safi na si kukusanya fedha pekee huku akiwaambia wananchi, “kama kuna mtu anataka kuhama Geita, mwambie ahairishe kwani yajayo si tu kufurahisha, bali yatashangaza”, huku akiwahakikishia usalama wa fedha za miradi ya jamii CSR zinazoendelea kuleta matokeo chanya ndani ya mwaka mmoja tangu kuteuliwa kwake.
Alihitimisha kwa kutoa namba yake ya simu akiwaambia wananchi waitumie kumwambia wanaowapa wanafunzi mimba, wazazi wanaowatumikisha watoto wa umri wa kwenda shule, watumia dawa za kulevya, vibaka na majambazi ili ashughulike nao akiwa kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama.
Kwa upande wake Bw.Pancras Shwekelela, Afisa Mazingira kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mji Geita amewaambia wananchi kuwa, tayari yamefanyika mabadiliko ya sheria ya mazingira hivyo wajiandae kuipokea na kuitekeleza sheria hiyo mara itakapoanza kutumika kwa lengo la kuboresha usafi wa mazingira.
Mkurugenzi wa kampuni ya usafi Bw. Godwin Bagandanshwa na meneja wake Bw. Sixbert Tibaijuka wamemhaidi mkuu wa mkoa kufanya kazi kwa uaminifu huku wakiomba ushirikiano uendelee kutolewa na wananchi ili kurahisisha kazi wanayoifanya.
Awali Afisa Tarafa Geita Mjini Bw. Innocent Mabiki aliwashukuru wananchi kwa kuitikia wito huo na kuwaomba kulifanya zoezi hilo kuwa endelevu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa