Mkuu wa mkoa wa Geita mhe.mhandisi Robert Gabriel amewataka wataalam ndani ya mkoa wa Geita kuwa na utamaduni wa kutumia takwimu ili kuwa na mipango bora itakayowezesha ufanisi wa kazi katika kutekeleza shughuli mbalimbali ili kuepuka kwenda bila mwelekeo katika kufikia malengo yaliyowekwa kiutendaji.
Ameyasema hayo Aprili 22, 2021 alipokuwa akiendelea na ziara yake kwenye jimbo la Geita Mjini hususan halmashauri ya mji Geita, ikiwa ni halmashauri ya mwisho kulitembelea ndani ya mkoa katika ziara yake mkoa mzima aliyoiita ni ya uamsho kwa kusudi la kuwakumbusha watendaji kutekeleza wajibu wao, kujadili changamoto na kuzitatua ili kuinua kiwango cha ufaulu kwa kuboresha miundombinu lakini pia kuinua ari ya walimu ikiwa ni pamoja na kuwapa motisha mbalimbali pamoja na kuupongeza mgodi wa GGML, Mbunge wa Geita Mji,uongozi Halmashauri ya Mji Geita, Madiwani, wananchi na wadau mbalimbali wanaochangia maendeleo ndani ya Geita
“sasa ni wakati wa kuhakikisha tunatumia takwimu ili zitusaidie kupanga mipango yetu kwani huwezi kuwa na mipango bila vigezo, hii itatusaidia kuwa na makisio halisia na kutatua changamoto ya vyumba vya madarasa, viti na meza, tukitambua kwamba kufikia mwaka 2023 idadi ya wanafunzi walio shule ya msingi itaongezeka kutokana na mwitikio uliotokana na elimu bila malipo”, amesema Mhandisi Gabriel
Mhandisi Gabriel ameelekeza uongozi wa kata na mitaa au vijiji ndani ya Geita kuwa na mikakati ya ujenzi wa nyumba za watumishi, matundu ya vyoo mashuleni pamoja na mabweni ikiwa ni hatua za kupunguza umbali kwa wanafunzi lakini pia kuhimiza kutokomeza madaraja (division) IV na 0 kwenye matokeo ya madarasa ya mitihani ya kidato cha pili na cha nne hivyo kuinua kiwango cha ufaulu.
Katika upande mwingine, mhandisi Gabriel amesikitishwa na idadi ya wanafunzi watoro kwa baadhi ya shule huku akikemea utoro wa jumla na rejareja, akionya na kuwataka wazazi wa watoto hao waelezwe juu ya sheria zitakazowatia hatiani endapo hawatawapeleka watoto wao shule, huku akihimiza watendaji kufahamu sababu halisi zinazochangia utoro ikiwa si wote ni watoro bali wengine ni wagonjwa, wamehama n.k hivyo kupunguza idadi inayoripotiwa kuwa ni kubwa.
Katika ziara hiyo, Mwalimu wa kujitolea wa somo la hesabu Secilia Nyalinga aliweza kujinyakulia zawadi kutoka kwa mkuu wa mkoa alipojibu swali lililoulizwa kwa waalimu wa hesabu katika shule ya sekondari ya Shantamine iliyopo halmashuri ya mji Geita ambapo mkuu wa shule hiyo pia alipongezwa kwa utendaji wake kwa kuwa shule hiyo ni miongoni mwa shule 3 zisizo changamoto nyingi kama shule nyingine alizozitembelea.
Ziara hiyo ilijumuisha kuitembelea shule ya sekondari shantamine, kuweka jiwe la msingi zahanati ya mgusu, kutembelea shule ya sekondari mgusu, shule ya sekondari kalangalala, kuweka jiwe la msingi shule ya sekondari kisesa pamoja na kuitembelea shule ya sekondari bombambili.
Kazi inaendelea.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa