Mkoa wa geita umezindua maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa mwaka 2019, ambapo miongoni mwa malengo ya wiki hii yamejikikita katika kuinua uelewa wa jamii kuhusu usawa wa kijinsia, sheria zinazowezesha kulinda, kuendeleza, na kusaidia unyonyeshaji wa maziwa ya mama na hivyo kuboresha lishe ya watoto na jamii.
Uzinduzi huo umemefanyika Agosti 2, 2019 katika eneo la kituo cha afya Katoro kilichopo mamlaka ya mji mdogo katoro, halmashauri ya wilaya ya geita, ambapo mgeni rasmi Bw. Vunza Mohamed kwaniaba ya Mganga mkuu wa mkoa, katika hotuba yake ameeleza imani aliyonayo kwa wadau mbalimbali wa lishe na waandishi wa habari kutumia ujuzi na taaluma walionayo kuhamasisha na kuelimisha umma kuhusu utunzaji wa ustawi wa watoto hasa wale wachanga na wadogo kwani ni jukumu la kila mmoja na kuwashukuru wadau wa Mradi wa USAID Boresha Afya kwa kuwa wadau muhimu kwenye utekelezaji wa maadhimisho ya wiki hii.
Amesema, “kwakuwa wiki hii huadhimishwa kila mwaka tangu mwaka 1992, ni vyema sasa tuungane kwa pamoja katika kukumbushana umuhimu wa kuendeleza na kuimarisha unyonyeshaji maziwa ya mama kama njia bora zaidi ya kujenga afya ya mama na mtoto kimwili na kiakili”
Bw. Mohamed amesisitiza kuwa, bado takwimu za unyonyeshaji za mkoa zipo chini licha ya kuwepo kwa elimu mbalimbali za unyonyeshaji wa maziwa ya mama kupitia vituo vya kutolea huduma za afya na wahudumu wa afya ngazi ya jamii, kwani ni asilimia 71 tu ya watoto wenye umri chini ya miezi sita wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee wakati asilimia 40.7 wakiendelea kunyonyeshwa maziwa ya mama mpaka wanapofikisha umri wa miezi 24, kisha kukata utepe ishara ya kuzindua wiki hii.
Akikagua banda la lishe, Bw.Mohamed amewasisitiza akina mama kuhakikisha mtoto mchanga wa umri chini ya miezi sita anakunywa maziwa ya mama pekee na si vyakula vya kawaida ili kuijenga lishe yake kuepuka udumavu.
Kwa upande wake Bw.James Katto ambaye ni mwakilishi wa mratibu Mradi wa USAID Boresha Afya Mkoa wa Geita amesema, wao wanaungana na wadau wa lishe nchini na nchi nyingine duniani kuadhimisha wiki hii wakijua kuwa, maadhimisho haya yamelenga kusisitiza juu ya umuhimu wa kulinda, kuimarisha na kuendeleza unyonyeshaji maziwa ya mama.
Bw.Katto ameendelea kusema, tafiti za kidemografia za mwaka 2015/16 zinaonesha kwamba, asilimia 38.9 ya watoto chini ya miaka 5 kwa mkoa wa Geita wamedumaa, kiwango ambacho ni kikubwa ukilinganisha na kiwango cha kitaifa ambapo ni asilimia 31.8, udumavu unaochangiwa na lishe duni kipindi cha ujauzito hadi mtoto anapofikisha umri wa miaka miwili. “Hivyobasi katika maadhimisho ya wiki hii, Mradi USAD Boresha Afya utawezesha watoa huduma katika vituo vya afya kutoa elimu ya lishe, kutathimini hali ya lishe ya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano na kutoa ushauri wa afya na lishe kwenye jamii” alimaliza Bw.Katto.
Hivyo, wito umetolewa kwa wananchi wote mkoani Geita kutumia fursa hii muhimu ya wiki ya unyonyeshaji kufika katika vituo vya afya kupata ushauri wa kitaalam kuhusu afya na lishe kwa ujumla na kutambua hali yao ya lishe.
Akitoa neno la shukrani, mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya geita dkt.Raphael Mhana, amewashukuru wadau wa mradi wa USAID Boresha Afya huku akiwasihi akinamama kuhakikisha wanaiandaa afya ya mtoto mapema kwani inaanza kabla ya kubebwa ujauzito na hata baada ya mtoto kuzaliwa basi wahakikishe mtoto ananyonya maziwa ya mama kwa miezi sita ya kwanza bila kupewa chakula kingine.
Kwa mwaka 2019, Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani yameanza Agosti 1, 2019 na yatakamilika Agosti 7, 2019 na kwa mkoa wa Geita yatafanyika kwenye halmashauri zote kupitia vituo vya kutolea huduma za afya.
Ni muhimu wanajamii kupewa taarifa sahihi ili kuwasaidia wanawake wote waweze kunyonyesha na kuwatunza watoto wetu ili hatimaye tupate taifa lenye watu bora zaidi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa