Wananchi waishio katika mkoa wa Geita wamehamasishwa kutumia nishati mbadala ya gesi katika kupikia pamoja na mkaa mbadala ili kutimiza agizo la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linalosisitiza matumizi ya nishati safi na salama ili kupunguza uharibifu wa mazingira.
Hamasa hiyo imetolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa 2025 Ndugu. Ismail Ali Ussi kwa nyakati tofauti katika Halmashauri Zote za Mkoa wa Geita wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ulioanza mbio zake ndani ya Mkoa huo kuanzia tarehe 01 hadi 06 Septemba 2025.
Ndg. Ismail Ali Ussi ameeleza kuwa maeneo mengi ya Nchi yetu yamekumbwa na janga la uharibifu wa mazingira hususan ukataji miti kwa lengo la kuchoma mkaa na kupata kuni za kupikia majumbani, hali ambayo inahatarisha uendelevu wa uoto wa asili na athari nyingine zinazotokana na ukataji miti hovyo, Hivyo wananchi wote mnatakiwa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kutumia nishati ya gesi.
Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Ndg. Philip Makungu amesema kuwa wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, Halmashauri yake imegawa mitungi 100 kwa makundi maalum ambapo mitungi 50 imegawiwa kwa mama lishe katika Kata ya Makurugusi na mitungi 50 katika Kata ya Chato na Muungano. Pia mitungi 400 itauzwa na Wakala wa Nishati Vijijini( REA) kwa bei ya punguzo ili kuwezesha wananchi wa hali mbalimbali kumudu gharama hiyo.
Ndg. Philip Makungu ameongeza kuwa sambamba na zoezi la ugawaji wa mitungi ya gesi Wilaya imeendelea kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi na bora hasa gesi, umeme na majiko banifu ya kupikia katika maeneo ya wachimbaji wadogo, shule na vyuo vilivyoko wilayani Chato. Pia wanaendelea kushirikiana na REA kuuza mitungi kwa bei ya punguzo pamoja na kuhimiza Taasisi zenye watu Zaidi ya 100 kutumia nishati safi katika kupikia.
“Kupitia kampeni ya matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia, manufaa mbalimbali yamefikiwa ikiwa ni pamoja na Taasisi mbalimbali kuanza kutumia mfumo wa nishati safi na salama, Kuwafikia wachimbaji madini 126 na kuwahamasisha kutumia umeme wa petrol au dizeli katika kutoa maji kwenye mashimo pamoja na kutoa elimu katika shule 10 za Sekondari ili kutunza mazingira na bionuai kwa vizazi vya sasa na vya baadae.” Aliongeza Ndg. Philip Makungu.
Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 zimeongozwa na kauli mbiu isemayo “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa