Jamii ya wafugaji wa mnyama punda katika Mkoa wa Geita wameaswa kuhakikisha wanajali haki na afya ya mnyama huyo.
Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Shirika la Arusha Society for the Protection of Animals (ASPA) Ndugu.Livingstone Masija alipokuwa akizungumza na wadau mbalimbali wa kutetea haki za mnyama punda kwenye kikao kazi kilichofanyika katika Kata ya Mgusu Manispaa ya Geita tarehe 11 Septemba 2025.
Ndg. Masija ametaja haki tano za wanyama kuwa ni uhuru dhidi ya njaa, kiu na utapiamlo, uhuru dhidi ya hofu na dhiki, uhuru dhidi ya maumivu, majeraha na magonjwa pamoja na uhuru wa kufanya na kuonyesha matendo na tabia za asili.
Mkurugenzi wa Shirika la ASPA ameeleza kuwa lengo kuu la kwenda kuwatembelea punda katika maeneo wanayofanya kazi ni kuwapima afya zao kabla ya kuwaanzisha matibabu ya magonjwa mbalimbali yanayowasumbua kama vidonda, minyoo na homa na kuangalia maendeleo ya ustawi wa mnyama punda tangu walipotoa elimu.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Chama cha Ushirika Mgusu ambao ni wadau wanaomtumia mnyama punda katika kazi zao za kubeba mawe madogo na udongo wenye dhahabu kutoka eneo la machimbo hadi kiwandani kila siku, Mjumbe wa Bodi ya Chama hicho Bw. Erick Joseph amesema kuwa tangu wapatiwe elimu na Shirika la ASPA juu ya utunzaji wa mnyama huyo wanajali afya na haki za punda na kuwapatia muda wa kutosha wa kupumzika.
Dkt. Jasson Mutayabarwa, Daktari wa nyama Halmashauri ya Manispaa ya Geita amesema kuwa wataalam wa tiba za mifugo katika Wilaya ya Geita wamenufaika na shirika la ASPA baada ya kuwezeshwa kuisaidia jamii kuondokana na dhana potofu juu ya matumizi holela ya dawa kwa wanyama hususan punda.
“Elimu inayotolewa na ASPA kwa wataalam wa mifugo na wafugaji imeleta mwamko mkubwa ambapo kwa sasa wafugaji wengi na wamiliki wa wanyama wanafanya mawasiliano na Maafisa mifugo walioko katika maeneo yao pale wanapohisi wanyama wao wana changamoto za kiafya na kupatiwa huduma ya vipimo na tiba sahihi.” Aliongeza Dkt. Mutayabarwa.
Kwa upande wake mfugaji wa wanyama punda Ndg. Simon Bukombe amesema kuwa hapo awali walikuwa wanawatumikisha punda kwa kuwabebesha mizigo mizito kuliko uwezo wao, kuwatandika viboko waliposhindwa kufanya kazi kulingana na matakwa ya wenye mizigo pamoja na kutowapa muda wa kupumzika. Lakini elimu waliyopatiwa na shirika la ASPA limewajengea uwezo wa kuwapenda, kuwajali na kuwapa punda muda wa kupumzika kuanzia saa 7 mchana ili wajenge afya zao.
ASPA ni shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu jijini Arusha, ambalo limejikita katika masuala ya ustawi wa wanyama hususan wasiopewa kipaumbele. Shirika hilo linafadhiliwa na Shirika la Brooke East Africa lenye makao yake makuu jijini Nairobi Nchini Kenya.
Shirika la ASPA linafanya kazi ya kupunguza mateso kwa wanyama kupitia elimu inayotolewa kwa makundi mbalimbali katika jamii kuanzia wanafunzi wa shule za Msingi pia limekuwa likitoa huduma za afya ya wanyama kwa Zaidi ya miaka 20.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa