Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 Ndugu Ismail Ali Ussi ametoa pongezi kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kwa kuwa wabunifu kwa kutunza vyanzo vya maji ambavyo vimeleta ahueni kwa wananchi kupata maji kwa ajili ya kunyweshea mifugo pamoja na matumizi mbalimbali ya nyumbani.
Ndg. Ismail Ali Ussi ametoa pongezi hizo tarehe 6 Septemba 2025 Mwenge wa Uhuru ulipotembelea chanzo cha maji mto Mtakuja kilichopo katika Shamba la miti Silayo Kata ya Minkoto Wilayani Chato na kuzindua kampeni ya upandaji miti katika chanzo hicho.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2025 ameeleza kuwa TFS wana jukumu la kusimamia uhifadhi wa misitu lakini wamejiongeza na kuwa wabunifu katika kutoa faraja na upendo kwa wananchi wa Kata ya Minkoto na maeneo jirani kwa kutunza vyanzo vya maji.
Akitoa taarifa ya mradi huo kwa niaba ya Mkuu wa shamba la miti Silayo, Bw. Lwamuhoza Elizeus amesema chanzo cha maji mto Mtakuja ni moja kati ya vyanzo vya maji Zaidi ya 14 vilivyopo ndani ya shamba la miti Silayo kikitiririsha maji yake kuelekea Kijiji cha Minkoto.
Bw. Lwamuhoza Elizeus ameongeza kuwa chanzo hicho kilichoanza kufufuliwa na kuzalisha maji kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 kimewanufaisha wananchi takribani 2000 wa vitongoji vya Mtakuja, Usukumani, Mwabasabi na Nyalubere katika kijiji cha Minkoto ambao wanapata maji ya kutosha kwa matumizi ya kila siku kama kunywesha mifugo, kupikia, kufulia na kuendesha shughuli za kilimo cha umwagiliaji kupitia maji yanayotiririka.
“ Baadhi ya faida zilizopatikana kutokana na uwepo wa chanzo hiki ni pamoja na wananchi wa kijiji cha Minkoto hususan wanawake wamepunguziwa umbali wa kwenda kutafuta maji kutokana na upatikanaji wa maji ya uhakika, kuchangia uhifadhi wa uoto wa asili, kudumisha mfumo wa ikolojia katika eneo la hifadhi, kusaidia uoteshaji wa miche na ukuzaji wa miti ambayo hutolewa bure kwa wananchi.” Aliongeza Bw. Lwamuhoza Elizeus.
Bw. Lwamuhoza Elizeus ameeleza kuwa mpango endelevu wa TFS ni kuongeza kasi ya uhifadhi wa vyanzo vya maji kwa kupanda miti rafiki kwenye vyanzo vya maji, kutoa elimu ya uhifadhi wa vyanzo vya maji kwa wananchi, kuchukua hatua za haraka juu ya shughuli yoyote inayohatarisha uhai wa vyanzo hivyo vya maji, kuendelea kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Chato katika kutekeleza mikakati endelevu ya utunzaji wa vyanzo vya maji vilivyopo ndani na nje ya hifadhi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa