Mkoa wa Geita una eneo linalofaa kwa kilimo jumla ya hekta 1,402,000, eneo linalolimwa ni wastani wa hekta 661,266.5. Mazao Makuu ya Chakula yanayolimwa katika Mkoa wa Geita ni Mahindi, Mpunga, Mtama, Mihogo, Maharage na Viazi vitamu. Mazao haya pia hutumika kama Mazao ya Biashara. Mazao Makuu ya Biashara ni Pamba, Alizeti, Tumbaku, na Nanasi.
Mkoa hupata mvua kiasi cha mm 900 hadi 1200mm kwa vipindi viwili vya Vuli na Masika. Mvua za Vuli huanza mwezi Septemba hadi mwezi Januari na mvua za Masika huanza mwezi Februari hadi Mei.
Uzalishaji wa mazao ya chakula msimu wa kilimo 2021/2022
Kwa ujumla katika msimu wa Kilimo 2021/2022, uzalishaji wa mazao ya chakula ulikuwa wa kuridhisha. Katika msimu wa kilimo 2021/2022 Mkoa wa Geita ulilenga kulima hekta 605,575 za mazao ya chakula zilizotarajiwa kuzalisha tani 1,704,183. Katika msimu huu, jumla ya hekta 574,137 zililimwa mazao ya chakula sawa na 94.8% ya malengo ambazo zimezalisha jumla ya tani 1,608,788.2 za mazao ya chakula.
Uzalishaji wa mazao ya biashara msimu wa kilimo 2021/2022
Katika msimu wa kilimo 2021/2022 Mkoa ulilenga kulima jumla ya hekta 72,997 kwa lengo la kuzalisha tani 137,351. Aidha, eneo lililolimwa lilikuwa ni hekta 48,946 sawa na 67% na kuzalisha tani 77,663.
Hali ya usalama wa chakula msimu wa kilimo 2021/2022
Kwa ujumla hali ya chakula ilikuwa ni ya utoshelevu. Kulingana na uchambuzi uliofanywa na Wizara ya Kilimo, Mahitaji ya Chakula kwa Mkoa ni tani 582,316 uzalishaji wa jumla kwa kufuata kigezo cha ulinganifu wa nafaka (grain equivalent) ni tani 699,957. Kwa mantiki hiyo ziada ya chakula kwa Mkoa ni tani 117,659. Ziada hii ni ndogo ikilinganishwa na ziada ya msimu wa 2020/2021 ambapo ziada ilikuwa tani 129,882.
Malengo ya kilimo msimu wa kilimo 2022/2023
Katika msimu wa kilimo 2022/2023 Mkoa umelenga kulima jumla ya hekta 577,394 kwa lengo la kuzalisha tani 1,631,070 na hekta 83,317 za mazao ya Biashara kwa lengo la kuzalisha tani 165,000. Mpaka kufikia 31/12/2022 jumla ya hekta 373,938 sawa na 64.7% ya malengo za mazao ya chakula zilikuwa zimelimwa na hekta 57,945 za mazao ya biashara zilikuwa zimelimwa.
Katika msimu wa kilimo 2021/2022 Mkoa ulilenga kulima Hekta 60,675 sawa na Ekari 151,687.5 zilizokadiriwa kuzalisha tani 70,004 za Pamba kwa wastani wa kilo 500 kwa ekari moja. Jumla ya Kilo 13,362,330 sawa na tani 13,362.6 zimevunwa. Thamani ya Pamba hii ni Tsh. 22,759,320,430 ambapo Halmashauri zetu zilitarajia kupata ushuru utokanao na mauzo ya Pamba kiasi cha Tsh. 682,779,613
Katika msimu wa kilimo 2022/2023 Malengo ni kulima Hekta 54,641 sawa na Ekari 136,602.5 zinazotarajia kuzalisha kilo 69,368,000 sawa na Tani 69,368. Hadi sasa jumla ya hekta 47,555 sawa na 87 % ya malengo zimelimwa na kupandwa pamba.
Mahitaji ya Mbegu ni tani 1366.02, mahitaji ya Viuadudu ni Ekapaki 546,410 na. Hadi kufikia tarehe 31/12/2022, jumla ya tani 1,873 za mbegu bora ya pamba zilikuwa zimesambazwa katika Halmashauri na vinyunyizi Ekapaki 66,500.
Alizeti ni zao la Kimkakati la Kimkoa ambapo lengo ni kutatua changamoto ya nakisi ya mafuta ya kula, kufungamanisha na Sekta ya Mifugo na kuongeza kipato na ajira kwa wananchi.
Kwa kutambua umuhimu huo, Mkoa umechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa zao la Alizeti linapewa kipaumbele miongoni mwa wakulima na wadau wote. Baadhi ya hatua hizo ni pamoja na: - Kuhamasisha kilimo cha zao la alizeti katika kila Halmashauri, kubaini wakulima watakaolima zao la alizeti katika msimu wa 2022/23 na kubaini maeneo yatakayolimwa alizeti kwa kila Halmashauri. Hadi kufikia tarehe 31/12/2022, Jumla ya Wakulima 6,323 na eneo la ekari 11,896 limebainishwa kwa ajili ya kilimo cha alizeti. Hata hivyo Mkoa umeshazielekeza Halmashauri kufanya maandalizi ya upatikanaji wa mbegu bora za alizeti ili wakulima waweze kuzipata kwa urahisi katika maeneo yao. Maandalizi hayo ni pamoja na kubaini mahitaji halisi ya mbegu kulingana na ekari zilizobainishwa, kuhakikisha mbegu hizo zinatoka katika chanzo sahihi cha uzalishaji wa mbegu bora na kuhakikisha mbegu hizo zinapatikana kwa bei himilifu kwa wakulima.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa