Mkoa wa Geita unazo fursa mbalimbali za Kiuchumi ambazo kimsingi ndizo zimekuwa zikichochea ukuaji wa sekta ya viwanda katika mkoa. Fursa hizo za Kiuchumi zimejikita katika shughuli kuu za uzalishaji mali za kilimo, ufugaji, uchimbaji madini ya dhahabu, uvuvi na baishara ndogondogo. Mkoa unatekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwa na Uchumi wa Viwanda hususani viwanda vidogo katika Mkoa ni sekta muhimu katika kutengeneza ajira, kukuza kipato na kuondoa umasikini.
Mkoa una jumla ya viwanda 791, ambapo viwanda viidogo ni 521, vya kati ni 269 na viwanda vikubwa vitatu (03). Sekta ya kilimo ndio inayoongoza kwa uwekezaji wa viwanda vya usindikaji wa mazao hususan mazao ya nafaka hasa usindikaji wa mahindi ukifuatiwa na zao la mpunga. Aidha, uwekezaji mkubwa ni shughuli ya kukoboa mpunga na kusaga mahindi ambapo kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 1 inakadiriwa kuwekezwa.
Sekta mpya katka uwekezaji wa viwanda ni pamoja na usindikaji wa mafuta ya alizeti na unenepeshaji wa mifugo hususan ng’ombe wa nyama unaofanyika wilayani chato. Pia zao la Pamba limeonesha kufufua matumaini ya uwekezaji katika viwanda vya kuchambua pamba ambapo mkoa una jumla ya viwanda (02) vya kuchambua Pamba vinavyofanya kazi, viwanda hivyo ni KCCL kilichopo wilaya ya Geita na BCU katika Wilaya ya Chato.
Shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO)
Mkoa unayo Ofisi ya kuhudumia viwanda vidogo ambayo imeanzishwa mwezi Desemba 2015. Katika kutekeleza majukumu yake Ofisi hiyo imekuwa ikitoa huduma mbalimbali kwa wajasiriamali kama ifuatavyo:-
Kuendeleza/ Kuleta teknolojia mbalimbali katika Mkoa huu kama vile mitambo ya kusindikaalizeti na utengenezaji sabuni.
Mkoa unayo mikakati ifuatayo katika kuendeleza sekta ya viwanda:-
Kuanzisha kiwanda cha kuchakata muhogo na kufungasha ambapo maghala (02) ya kuhifadhi muhogo na soko (01) yamejengwa na Kukamilika kupitia Programu ya uboreshaji wa miundombinu ya masoko uongezaji thamani na huduma za kifedha vijijini (MIVARF). Vikundi vya wazalishaji vimekutanishwa na benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB) kwa ajili ya kupewa mkopo na andiko la Mradi linaandaliwa.
Kufufua kiwanda cha kuchambua Pamba cha Kasamwa Geita ambapo hatua iliyofikiwa sasa ni kuwa NCU (1984)LTD inashirikiana na Mifuko ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya kufunga vyerehani vipya 20 aina ya Bajaj ili Pamba iliyozalishwa msimu huu 2017/2018 iweze kuchambuliwa.
Kuhamasisha na kuandikisha Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Geita ambacho kitahusisha Wilaya za Geita, Nyang’hwale, Bukombe na Mbogwe kwa ajili ya kusogeza huduma za uzalishaji wa mazao ya biashara kwa wakulima na kuboresha masoko ya mazao yao.
Kuanzishwa kiwanda cha kusindika nyama katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe ambapo andiko limeandazliwa na kuwasilishwa katika Wizara ya Viwanda, Biashara na uwekezaji kwa ajili ya kupata mwekezaji.
Ujenzi wa Kiwanda cha sukari Nyamwilolelwa/Chigunga eneo la ekari 100 limetengwa na serikali ya kijiji cha Chigunga. Eneo la hekta 6,000 sawa na ekari 14,826 zinazomilikiwa na wakulima zitatumika kuzalisha miwa. Halmashauri ya wilaya ya Geita imetenga shilingi bilioni 1.402 kwa ajili ya kiwanda hicho mwaka 2018. Kiwanda kitaendeshwa kwa ubia baina ya Halmashauri ya Wilaya na Bodi ya sukari Tanzania.
Kuanzisha kiwanda cha kufungasha mazao ya nyuki (Asali na Nta)_ katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe. Uhamasishaji wa vikundi vya wafugaji wa nyuki kujiunga pamoja ili vitambulike kisheria na viweze kukidhi vigezo vya kukopsheka umefanyika.
Kutangaza fursa za kilimo cha mpunga kwenye mabonde yaliyopo wilaya ya Chato na Geita kwa wawekezaji ambao wako tayari kuweka miundombinu ya umwagiliaji kwa kutumia maji ya ziwa Victoria.
Kuanzishwa kwa Supermarket katika Mji wa Geita ambayo itauza bidhaa za viwanda vidogo zinazozalishwa na wajasiriamali wa Mkoa wa Geita. Eneo limeshapatikana katika soko jipya linalojengwa katika mjia wa Geita.
Uanzishwaji wa kiwanda cha Nyama – Chato ambacho kinaanzishwa na Kampuni ya Kahama oil Mills (KOM) ambapo eneo la ekari 1000 limepatikana katika kijiji cha Itale kiwanda kitapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 700 kwa siku.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa