Katika kuhakikisha watumishi wa Umma Mkoani Geita wanafanya kazi na kuleta matokeo, Katibu Tawala Mkoa wa Geita Bw. Denis Bandisa amekutana na kufanya kikao na Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita tarehe 08.10.2018 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Hiki ni kikao cha kwanza cha Kimkakati ambacho Bw. Bandisa anakitumia kuwahamasisha watumishi kufanya kazi kwa bidii ili kutekeleza Dira na Dhima ya Mkoa ambayo hupelekea matokeo kwenye utekelezaji wa shughuli za serikali na kuwahudumia wananchi.
Amesema, “moja ya mambo yanayopelekea mafanikio ni Ushirikiano, kwakuwa watu wanaoshirikiana hujenga, ni rahisi kufanikiwa kwa kuwa kila mmoja atajiona ni mhusika, hivyo nahimiza ushirikishwaji baina ya idara na idara ili kila mmoja apte nafasi ya kutoa matokeo”.
Ameongeza kusema kuwa, watumishi wa Umma sharti wawe na Weledi na Ujuzi hata kwa kuongeza elimu. Amewashauri kupenda kujiendeleza kielimu kwakuwa elimu haina mwisho, vilevile hata wanaopenda kupandishwa vyeo ni muhimu kujiimarisha kitaaluma.
Bw. Bandisa pia amewakumbusha watumishi juu ya kuwa na nidhamu kazini, tabia nzuri, majibu mazuri kwa wateja na kusema kuwa unyenyekevu ni dawa pale unapomhudumia mteja ama mwananchi.
Mwisho, watumishi wamehimizwa juu ya uwazi na kutokuwa wabinafsi katika kutumia rasilimali zilizopo katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku bila kusahau uwajibikaji akisisitiza kuwa unaanzia hata nyumbani kwamba, kama hata mtoto asipofundishwa vizuri tangu angali mdogo ni vigumu kuwajibika hata akiwa mkubwa kwa kuwa siku zote yatupasa kutambua kuwa, “HAKUNA HAKI BILA WAJIBU”, kisha akakalibisha michango na changamoto kutoka kwa watumishi hao.
Watumishi wakampongeza Bw. Bandisa kwa kufanya kikao pamoja nao wakisema kuwa huu ni mwanzo mzuri kwakuwa endapo watakuwa na changamoto wataziwasilisha kwa ajili ya utatuzi ikiwa lengo lao ni kuufikisha mkoa kwenye malengo uliojiwekea katika kufikisha huduma kwa jamii pia wakaahidi kufanyia kazi yote waliyoelekezwa.
Hakika Geita ni ya Amani, Umoja na Kazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa