Na Boazi Mazigo-Geita RS
Katika sura ya kwanza, ibara ya 9 (D)(i) ya ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 imeeleza wazi juu ya Kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za Afya, Elimu, Maji, Umeme na Makazi vijijini na mijini ikisema, “Kuongeza kasi ya usambazaji majisafi na salama ili kutosheleza mahitaji kwa zaidi ya asilimia 85 vijijini na zaidi ya asilimia 95 kwa mijini, kwa upande wa Tanzania Bara, ifikapo mwaka 2025, na zaidi ya asilimia 95 kwa upande wa Zanzibar”. Sura hiyo imeifanya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa Geita kupita, kutembelea na kujionea hali ya utekelezaji wa mradi wa majisafi wa miji 28 unaotekelezwa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo kupitia program ya Maendeleo ya sekta ya maji nchini (WSDP 2006-2025) kwa gharama ya Dola za kimarekani Milioni 16.493 sawa na shs.bilioni 38, mradi ulioanza Aprili 11, 2023 na kutarajiwa kumalizika Desemba 10, 2025.
Kamati hiyo iliyotembelea eneo la mradi Agosti 24, 2023 imesema, ipo haja ya kupanua zaidi huduma hiyo ya maji tofauti na ilivyokuwa imekisiwa kutokana na kuonekana fedha hiyo inaweza kuhudumia eneo kubwa zaidi ya lile lililoanishwa.
Akiongea akiwa kwenye eneo la mradi, mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM Mkoa Geita Nicholaus Kasendamila alisema, " nikupongeze mkuu wa wilaya mhe.Deusdedith Katwale pamoja na wizara ya maji kwa kuona umuhimu wa kusogeza huduma ya maji mbele zaidi ya mradi ulipokuwa umekisiwa na kuwa na ndoto ya kufikisha maji hayo kata ya Bwanga. Pia hakikisheni hakuna mwananchi yeyote anadai fidia ili kazi ifanyike vizuri. mwisho nimpongeze kwa dhati Rais wetu Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali wananchi anaowaongoza wakiwemo wa mkoa huu na wilaya ya Chato pia, tuendelee kumuunga mkono"
Akisoma taarifa ya mradi, afisa mazingira kutoka CHAWASSA bi. Jesca Salima alisema ujenzi wa mradi huo utahusisha ujenzi wa chanzo (Intake) chenye ukubwa wa lita 11,000,000 kwenye ziwa Victoria, ujenzi wa chujio (WTP) lenye ukubwa wa kuzalisha lita 10,000,000 kwa siku, ujenzi wa kuhifadhia maji eneo la Katende Hill lenye ujazo wa lita 3,000,000, ulazaji wa bomba kuu lenye kipenyo cha 300mm hadi 400mm urefu wa Km.36 kutoka chujio hadi kwenye tanki la Katende na kuyapeleka mjini kwenye matanki yaliyopo (Itale, Mlimani, Hospitali na Kiwandani pamoja na ulazaji wa mabomba ya usambazaji wa maji yenye vipenyo vya milimita 75 hadi 400 urefu wa km.30
Bi.Salima aliongeza kuwa, kata zitakazonufaika na mradi huo ni Ilemela, Katende, Ilyamchele, Bukome, Nyamigogo, Muungano, Chato, Bwina na Nyamirembe, na kwamba mradi utakapokamilika utaongeza upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kutoka asilimia 85 hadi 100 kwa mji wa Chato.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa