BODA BODA WASIOVAA KOFIA NGUMU GEITA KUKAMATWA
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi amemuagiza Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Geita Alfred Hussein kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria waendesha pikipiki wote wasiovaa kofia ngumu maarufu kama ''helmet'' wanapotimiza majukumu yao ya usafirishaji wa abiria.
Akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani ambayo kimkoa yanafanyika Mji mdogo wa Katoro Wilaya ya Geita Mheshimiwa Robert Gabriel amesema muendesha piki piki yeyeto asiyevaa kofia ngumu Mkoani humu akamatwe na kuwekwa ndani ili liwe fundisho kwa watu wote wasiopenda kutii sheria na matokeo yake wanasababisha vifo kwa jamii. "Naamini kuanzia wakati huu RTO na Kamati za Usalama barabarani Mkoa na Wilaya mtu asiyevaa kofia ngumu atakamatwa na kuwekwa ndani tutatumia sheria zote hakuna kupatana hakuna kuelewana". Ameongeza kuwa watumiaji wa vyombo vya moto wanatakiwa kuelimishwa na kufundishwa taratibu zinazowaongoza katika utumiaji wa vyombo hivyo na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi pamoja na vyombo vyao wapate elimu ili kujua mbinu za kuwafanya kuwa salama.
Mhandisi Robert Gabriel amewataka abiria kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama pamoja na kutowaruhusu madereva kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi kwa kuwa jukumu la Usalama ni la kila mwananchi.
Aidha, amekipongeza kikosi cha usalama barabarani mkoani hapa kwa kazi nzuri ya kuzingatia usalama wa wananchi katika barabara, amewataka waendelee kusimamia suala hili na kuchukua hatua pale inapobidi.
Awali Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani mkoani hapa ndugu Alfred Hussein alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa kuwa ajali za barabarani zimepungua kutoka ajali 87 mwaka 2016 hadi kufikia ajali 68 kwa mwaka huu. Vile vile ameeleza kuwa idadi ya vifo pia imepungua kutoka vifo 98 mwaka 2016 hadi vifo 79 kwa mwaka huu wa 2017.
Alfred ameongeza kuwa kwa ajali nyingi zinasababishwa madereva kuendesha vyombo vya moto wakiwa wametumia vilevi mbalimbali, mwendo kasi, kukosa umakini barabarani, uchakavu wa vyombo vya usafiri na miundombinu. Maadhimisho haya yanafanyika kwa wiki nzima ambapo wananchi, madereva na wamiliki wa vyombo vya moto wanapata elimu kwa lengo la kuhakikisha kila mtu anajikinga na ajali za barabarani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa