Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe.Rosemary Senyamule ameipongeza Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu ya Buckreef kwa uzalendo iliyouonesha mkoani Geita kupitia utoaji wa jumla ya Shilingi Milioni 321 kama fedha za wajibu wa kampuni kwa jamii yaani CSR zitakazotekeleza miradi ya elimu na afya katika halmashauri ya wilaya ya Geita ikiwa utekelezaji wa sheria inayowataka wamiliki wa makampuni ikiwemo migodi kudumisha mahusiano mema baina yao na jamii inayowazunguka, tukio lililofanyika Januari 27, 2022 ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Geita.
Akiongea baada ya kushuhudia utiaji saini makubaliano ya utekelezaji wa miradi hiyo, Mhe.Senyamule amewaelekeza Shirika la Madini la Taifa Mkoani hapa kuendelea kuwahamasisha na kuwaelekeza makapuni mengine nao kuwa na uzalendo kwa walionao Bucreef ili kuweza kuboresha maisha ya jamii ya Geita ili kuwa na uchumi imara hatimaye kuwa na uchumi wa juu.
“leo ni siku njema, kwanza kwa kusherekea kuzaliwa kwa Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kupitia maendeleo anayotuletea, lakini pia kwa kushuhudia utiaji saini baina ya halmashauri Ya wilaya ya Geita pamoja na Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu ya Buckreef. Ninawapongeza kwa kuwa mmeonesha utii wa sheria zinazoongoza uwekezaji na mmeonesha mpo tayari kuendeleza mahusiano na jamii inayowazunguka. Hivyobasi sisi kama serikali tutaendelea kuwapa ushirikiano na kupitia fursa hii niwaalike wengine nao kuiga mfano wa Bucreef na pia karibuni kuwekeza Geita, na haya ni matunda ya Geita ya Dhahabu, Utajiri na Heshima”, alisema Mhe.Senyamule
Mhe.Senyamule alimaliza kwa kuwasisitiza halamashauri kusimamia vyema ujenzi wa miradi hiyo ili kupata ubora na thamani ya miradi na kutumia muda vizuri ili miundombinu hiyo itow huduma kwa wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Buckreef ambaye ni Mkurugenzi wa TANGOLD Corporation Bw. Andrew Cheatle amesema, ni fahari kuwekeza Tanzania na kiu yao ni kuona maisha ya jamii yanaboreka akisema “ni heshima kutekeleza mpango wa CSR, hivyo ni imani yetu tukisaidia afya na ekimu kwa watoto wadogo tutakuwa tutafanikiwa, lakini pia kupitia kazi na ajira itasaidia kuinua uchumi wa jamii”
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt.Venance Mwasse amesema shirika hili lilianzishwa na kuingia kwenye shughuli hii kwaniaba ya Serikali na wananchi kwa ujumla. Ubia huo umeiletea serikali heshima kwakuwa wameacha alama, na kwamba wataendelea kuwasahuri na kuwaelekeza kutekeleza sheria, tumaini lao ikiwa ni kwamba huo utakuwa mgodi mkubwa muda si mrefu.
Akitoa maelezo ya namna ya utekelezaji wa makubaliano hayo, Meneja wa Buckreef Bw.Isaac Bisansaba amesema pamoja na uwepo wa sheria ya CSR, kampuni yao inawataka kufanya hivyo ambapo fedha iliyotolewa itaelekezwa kwenye kata nne za Kaseme shilingi milioni 75 ujenzi wa madarasa, Lwamgasa shilingi milioni 75 ujenzi wa maabara, Busanda shilingi milioni 75 kituo cha afya na Bugulula shilingi milioni 96 kituo cha afya kama miradi ya elimu na afya.
Viongozi wa wilaya kuanzia mkuu wa wilaya, mweneyekiti wa halmashauri, mkurugenzi pamoja na mwakilishi wa mbunge wa Busanda wamesema wanashukuru uwepo wa Buckreef kwakuwa wamekuwa ni watekelezaji wa sheria bila usumbufu wowote.
Katika uwekezaji wa Buckreef, STAMICO wanamiliki 45% na TANGOLD Corporation 55%
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa