Na Boazi Mazigo- Geita
Neema inaendelea kumwagika mkoani Geita kwenye awamu ya sita ya uongozi wa Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo viongozi mbalimbali wameshuhudia utiaji saini makubaliano ya utekelezaji mpango wa wajibu wa kampuni kwa jamii CSR ya shilingi milioni 420 kati ya Mgodi wa Bucreef unaojihusisha na uchimbaji madini ya dhahabu na halmashauri za wilaya na mji Geita.
Mkuu wa mkoa Geita Mhe.Martine Shigela ameshuhudia zoezi hilo Aprili 27, 2023 katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa na kuupongeza mgodi huo huku akitoa wito kwa wawekezaji wengine kuja kuwekeza mkoani hapa kisha kuagiza utekelezaji wa miradi ya CSR kuzingatia muda.
“hongereni sana Bucreef, hii ni fursa ya wanaGeita kuchangamka, tusizubae, tutumie fursa ya utekelezaji miradi ya CSR tuwe kwenye mnyororo wa thamani. Haya ni matokeo ya kupanua uwekezaji na juhudi hizi zinahimizwa na Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ambayo hata sisi Geita tumeendelea kufanya hivyo. Matarajio yangu ni kuwa, miradi iliyosainiwa leo itakamilika kabla ya mwezi novemba, 2023 na hata mchakato wa utekelezaji wa miradi ya CSR kutoka makampuni mengine ianze mapema mwishoni na mwaka huu”, alisema Mhe.Shigela
Aliongeza kuwa, mkoa utaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji na hivyo anatoa wito kuwaalika wawekezaji mkoani Geita kwa uwekezaji endelevu.
Meneja mkuu wa mgodi wa Bucreef Bw.Gaston Mujwahuzi alisema “tunaanza na CSR ya Milioni 420 kwa mwaka 2022/2023 na CSR yetu itahusika kwenye sekta ya elimu, afya na mazingira. Tunaamini mwakani kiwango kinaweza kuongezeka nasi tukachangia kiasi kikubwa kwa sababu kwa sasa tunazalisha Tani 45 kwa Saa kwa Sasa na mwaka 2024 tunatarajia kuongeza uzalishaji kufikia tani 90 hadi 100 kwa saa, hivyo tunaomba ushirikiano”
Kwa upande wake katibu tawala mkoa Geita Prof.Godius Kahyarara ameupongeza mgodi huo kwa kutekeleza mojawapo ya takwa la kisheria kuwajibika kwa jamii hivyo kusisitiza kuwa matokeo ni muhimu kwakuwa jamii inatarajia kuona kilichofanyika kutokana na makubaliano yaliyofikiwa kwenye utekelezaji wa miradi ya CSR.
Mkuu wa wilaya Geita Mhe.Cornel Magembe alitumia fursa hiyo kumpongeza Mhe.Shigela kwa kuwa sehemu ya kuwahimiza wawekezaji kutimiza jukumu hilo la kisheria akisema ni matarajio yake kuwa Bucreef pamoja na halmashauri za wilaya anayoiongoza watawajibika na kwamba wahakikishe miradi yote inatekelezwa na inakamilika kwa wakati akisema, “niko tayari kusimamia utekelezaji wa CSR hii”
Mgodi wa Bucreef unaundwa na Shirika la Madini la Taifa STAMICO kwa 45% na kampuni ya TRX Gold Canada kwa 55% na hufanya shughuli zake za uchimbaji wilayani Geita.
CSR Kututoa Kimasomaso Wana Geita
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa