Na Boazi Mazigo- Geita RS
Ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa Geita imeendelea ambapo Agosti 25, 2023 kamati hiyo imetembelea miradi mbalimbali ikiwemo jengo la wagonjwa mahtuti (intensive care unit) katika hospitali ya Nzera pamoja na jengo la ofisi ya makao makuu ya Halmashauri na kuonesha kuridhishwa na hatua za utekelezaji miradi hiyo.
Baada ya kupita na kukagua miradi yote, mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM Mkoa Geita Nicholaus Kasendamila alisema ameridhishwa kwa namna Halmashauri hiyo inavyosimamia miradi huku akitoa wito kwa Halmashauri zote kuendelea na utaratibu wa usimamizi ulio mzuri kisha kuendelea kumpongeza Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyowapambania wana Geita na watanzania kwa ujumla.
"niwapongeze na niwaambie sisi tumeridhika, kazi ni nzuri,hakikisheni mnamaliza kwa wakati ili jengo la makao makuu litumike kama ilivyopangwa na mwanzoni mwa mwezi Oktoba, 2023 tutaangalia kama kweli mmehamia. Pia niendelee kutumia fursa hii kumpongeza na kumshukuru sana Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyowapenda wananchi wake, anavyohangaika kutafuta fedha ili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, tumuunge mkono, tuisemee miradi"
Mwenyekiti Kasendamila vilevile akiwa kwenye miradi mingine ukiwemo wa Maji Busanda alipokea salamu nyingi za pongezi kwa serikali ya awamu ya sita kutoka kwa Wananchi akiwaomba pia kuendelea kuipokea miradi kuitunza na kuisemea kwa wanajamii wengine wapate kufahamu kazi kubwa inayofanywa na serikali inayoongozwa na CCM.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo la wagonjwa mahtuti (intensive care unit), mganga mkuu halmashauri ya wilaya Geita Dkt.Modest Buchard alisema, mradi huo uliletewa shilingi milioni mia tano (shs.500,000,000) ambapo unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 31, 2023 na tayari wamepokea vifaa tiba mbalimbali kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa mahututi ambavyo baadhi yake vimekwisha kufungwa. Aliongeza kuwa, kukamilika kwa jengo hilo kutaongeza ufanisi wa utolewaji huduma kwa wagonjwa katika mazingira mazuri yenye vifaa bora.
Kamati hiyo imetembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendelea ya sekta ya elimu, maji, maendeleo ya jamii, utawala na afya yenye thamani ya shs.3,725,306,474.95
Ziara ya kamati hiyo itaendelea Agosti 26, 2023 katika Halmashauri ya mji Geita
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa