Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Rosemary Senyamule amewaongoza wananchi wa Mkoa huo kupata Chanjo ya Ugonjwa wa Uviko 19 (Covid 19) leo tarehe 04 Agosti, 2021 kwenye hafla fupi ya uzinduzi iliyofanyika kwenye Ukumbi wa GEDECO mjini Geita.
Akizungumza kwenye Uzinduzi huo Mhe. Mkuu wa Mkoa ameishukuru serikali kwa kuwajali wananchi kwa kuwaletea Chanjo ili kuwakinga na Maradhi hayo yaliyo kwenye wimbi la tatu la maambukizi tangia kuibuka kwa ugonjwa huo mwaka 2019.
Aidha, Mhe. Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa wananchi kwenda kupata Chanjo hiyo kuanzia leo siku ya uzinduzi kwenye vituo vilivyobainishwa ambapo kwa Mkoa wa Geita wananchi wapatao elfu 50 watapata Chanjo hiyo kwa awamu ya kwanza kwenye vituo 18 yaani vituo vitatu kwenye kila Wilaya.
"Serikali yangu inajali na inawatakia mema watanzania wote, natoa wito kwa Makundi yote yaliyobainishwa kwa awamu ya kwanza kwenda kupata chanjo hii muhimu", amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Wilson Shimo pamoja na mambo mengine ametoa rai kwa wananchi kufanya mazoezi ya viungo na kuzingatia Lishe Bora kwa kula vyakula vyenye mlo kamili pamoja na vitamini C.
"Tunachokifanya hapa ni kwa maslahi ya Afya zetu, ..twendeni tukapate chanjo kwani pamoja maneno mengi yanayozunguka lakini hili tatizo lipo". amesema Mwinyiheri Baraza, kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa.
Askofu wa Kanisa katoriki Mkoa wa Geita, Flavian Kasala ametoa pongezi kwa serikali kwa uamuzi wa kuwapatia Chanjo ya Ugonjwa wa Uviko 19 ( Covid 19) na amewasihi wananchi kupata Chanjo ya Ugonjwa ili kulinda Afya zao. "katika awamu hii ya mzunguko wa tatu, tatizo hili limejidhihirisha kuwa ni kubwa sana," amesema.
"Ni nafasi kwa sisi kuonesha Imani kubwa kwenu katika kutusimamia kwani uwepo wenu ni kwa ajili ya Ustawi wa Taifa, kwani utaalamu wa kisayansi na Imani kwa viongozi wetu Mimi binafsi nakubali kuingia katika Chanjo na natoa wito kila mmoja ajitafakari na aone umuhimu na kupata Chanjo". Askofu Kasala.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Japhet Simeo amebainisha kuwa Chanjo ya ugonjwa wa Uviko 19 (COVID 19) inasaidia kupunguza uwezekano wa mgonjwa kupata dalili kali na hatarishi na inapunguza upotevu wa uhai wa watu. Aidha, Mganga Mkuu amesema Mkoani Geita jumla ya wananchi laki tatu watapata Chanjo hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa