Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amefungua kikao cha uhamasishaji wa zoezi la upuliziaji dawa ya Ukoko Majumbani kwa mara ya nne Wilayani Chato na mara ya tatu Wilayani Nyang’hwale katika Ukumbi wa Safety Park Hotel uliyopo Mjini Geita tarehe 23.08.2018.
Aemeanza kwa kutambua zoezi muhimu la upuliziaji dawa ya ukoko kwa kipindi cha sasa linalotegemewa kuendeshwa katika halmashauri za Chato na Nyang’hwale chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la Abt Associates kuanzia tarehe 24.10.2018 zoezi litakalodumu kwa siku 27. Amesema, anaamini kupitia jitihada na Mikakati ya pamoja, mafanikio ya kudhibiti ugonjwa wa Malaria kwa Mkoa wa Geita yatapatikana.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Mhandisi Gabriel ametoa msisitizo kwa viongizi akisema, “ni muhimu wananchi na jamii nzima wahimizwe juu ya matumizi sahihi ya vyandarua vyenye viuwatilifu kwa muda mrefu, upimaji na upatikanaji wa matibabu sahihi ya Malaria kwa wakati, viongozi kuanzia ngazi ya Kitongoji washiriki kufanya hamasa ili isivukwe hata nyumba moja katika zoezi hilo, kuhimiza matumizi ya tiba kinga kwa akinamama wajawazito bila kusahau kuzingatia usafi wa mazingira kwa ajili ya kuharibu mazalia ya mbu na kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya (ndani ya masaa 24 baada ya kupata homa)”.
Amewaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa, Serikali kupitia Mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria kwa ufadhili wa Mfuko wa Rais wa Marekani chini ya Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID), imekuwa ikitekeleza zoezi hilo katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa tangu mwaka 2010 na hivyo kutokana na mchango mkubwa wa kupunguza ugonjwa wa Malaria kwa kushusha kiwango cha maambukizi ya Malaria ulioonekana kwenye Halmashauri za Wilaya ya Butiama, Musoma Vijijini, Sengerema na Kwimba, ni vyema fursa hii ikatumiwa kipekee na Halmashauri zinazonufaika na zoezi hilo. Mkuu wa Mkoa pia amepongeza mpambano dhidi ya maambukizi ya Malaria kutoka asilimia 38.1 kwa mwaka 2015/16 na kufikia asilimia 17 katika taarifa ya utafiti ya viashiria vya Malaria na UKIMWI (Tanzania HIV Malaria Indicator Survey). Alimaliza kisha kukiweka kikao wazi kwa majadiliano.
Mratibu wa Malaria wa Mkoa wa Geita, Dkt. Mosses Simon akaeleza mafanikio yaliyopatikana ikiwemo upatikanaji wa dawa za mseto za kutosha pamoja na upimaji wa Malaria kwa asilimia 99 kutokana na uwepo wa vifaa vya kisasa na vinavyoweza kupima kwa haraka. Pia amesema Geita ina changamoto ya ugonjwa wa Malaria kutokana na hali yake ya hewa kuruhusu makuzi ya mbu hawa waenezao Malaria. La muhimu akaomba utungwaji wa sheria ndogo zitakazowawajibisha wale wote watakaokutwa wakitumia vyandarua kwa matumizi yasiyo sahihi.
Awali, Meneja Operesheni Kitaifa na Mwakilishi wa Abt sscociates ndugu Gaudence Juma alishukuru kwa ushirikiano ambao amekua akiupata kutoka serikalini na kwamba bila hivyo huenda zoezi lingekwama kwa nyakati zilizopita, hivyo kuomba ushirikiano kuanzia ngazi ya kitongoji uendelee kuwepo ili kurahisisha zoezi kufanyika kwa asilimia mia moja kwa kuwa zoezi litadumu kwa siku 27 ili kufikia lengo la asilimia 85 ya nyumba zote zenye sifa 177,053 ikiwa nyumba 119,726 ni za Chato na nyumba 57,327 ni za Nyang’hwale takwimu iliyotokana na nyumba zilizoachwa wakati wa zoezi awamu zilizopita.
Mratibu wa Abt Mkoa, ndugu Christopher Mshana Pia akagusia juu ya changamoto ya uelewa mdogo unaopelekea mgomo baridi wakati wa zoezi, ubadhilifu wa dawa, lakini pia kutotunza miundombinu ya upuliziaji dawa, jambo linalopelekea ufanikishaji zoezi kuwa mdogo.
Kwa upande wake mwakilishi wa Wizara ndugu. Peter Gitanya amekieleza kikao kuwa, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria ni kufikia chini ya asilimia moja ya maambukizi ya ugonjwa wa Malaria ifikapo mwaka 2020 ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) jambo ambalo linaonesha kufanikiwa.
Kisha Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa ndugu. Herman Matemu akaendesha mjadala uliochangiwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhe. Mhandisi Mtemi Msafiri ambaye kwa upande wake alihimiza wananchi wasio na ajira kushiriki zoezi hilo kwa asilimia mia moja na si kuwaweka watumishi kwenye nafasi nyingi wakati wa utekelezaji wa mradi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale Bi. Mariam Chaulembo naye akahimiza juu ya ushirikishwaji wa wananchi kuanzia mwanzo ili kufanikisha zoezi, na kwamba hii ndiyo fursa pekee kwa wananchi kunufaika.
Mwisho Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Japhet Simeo akahitimisha kwa kusema kuwa ni vyema kuhakikisha Wahe. Wakuu wa Wilaya husika wanawezeshwa kushiriki kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mradi lakini pia ratiba ya zoezi ifuatwe kama ilivyopangwa na kuwashukuru wadau kwa namna wanavyojitoa kuunga mkono juhudi za serikali.
Miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Wahe. Wenyeviti wa Halmashauri za Chato na Nyang’hwale, Maafisa Afya na Maafisa Habari.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa