Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, amemuapisha Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Mhe. Juma Said Nkumba tarehe 06.08.2018 na kumkaribisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita ndugu. Denis I. Bandisa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Josephat Maganga ambaye awali alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukombe katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Mhe. Mhandisi Gabriel, amewaeleza viongozi wote kwa ujumla wao kuwa yeye amejitolea mawazo, nguvu na akili ili kuiona Geita mpya inayomelemeta, hivyo kuwaonya viongozi kutoshiriki kupokea rushwa ya aina yoyote ile kwani kwa kufanya hivyo Geita mpya itakuwa ni historia tena na kuwaomba wasimwangushe Mhe. Rais kwani wao ndiyo wawakilishi wake kwa wananchi ndani ya mkoa. Akaongeza “nawaomba, nawaomba, naomba sana viongozi msikubali kuchafuliwa na rushwa, tuivunje hiyo laana”.
Baada ya kiapo hicho, Mhe. Said Nkumba amesema “nimepelekwa Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita kufanya kazi na viongozi na siyo makundi ya kisiasa, hivyo wenye makundi ya kisiasa wanipishe nifanye kazi”.
Mhe. Said Nkumba ameongeza kwa kusema kuwa anatambua kuwa Bukombe ni Wilaya ya Kilimo na yenye ardhi nzuri, hivyo atahakikisha anawatumia wataalamu wa kilimo waliyopo ili kuhakikisha ardhi kidogo, inatoa mazao mengi ili kuwanufaisha wananchi.
Kabla ya tukio hilo, Katibu Tawala aliyeteuliwa hivi karibuni ndugu. Denis I. Bandisa alitambulishwa kwa wajumbe na waalikwa waliohudhuria hafla hiyo, kisha akapata nafasi ya kusalimia.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Mhe. Martha Mkupasi akapata fursa ya kusema neno kwa niaba ya waheshimiwa wakuu wa wilaya wengine ambapo amehimiza ushirikiano baina yao ili kuleta maendeleo ndani ya mkoa ili kuipata Geita mpya.
Baada ya Hafla hiyo, Mkuu wa MKoa wa Geita, Mhe. Mhandisi Gabriel akaendesha kikao cha wadau wa elimu na afya kujadili juu ya mikakati ya kuondokana kabisa na upungufu wa miundombinu ya elimu na afya kabla ama ifikapo juni, 2019. Pamoja na masuala ya elimu na afya, Mkuu wa Mkoa alisisitiza juu ya kuwa na mpango mzuri wa matumizi ya ardhi na kuhimiza juu ya upangaji wa miji na kusema kuwa hatopenda kuona miji mipya ikikuwa pasipo kupangiliwa.
Amesisitiza pia juu ya ukusanyaji wa mapato kwa kuwa lengo la serikali ni Halmashauri kuweza kujitegemea na anaamini baada ya kumaliza changamoto ya upungufu wa miundombinu ya elimu na afya, kasi ya maendeleo itakuwa ni kubwa sana.
Miongoni mwa waliohudhulia hafla hiyo ni pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wahe.Wabunge, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi, Wakuu wa Idara na Vitengo,Makatibu Tawala Wilaya, Viongozi wa Dini, viongozi wa Taasisi mbalimbali za Umma na Binafsi, TSN, maafisa habari na waandishi wa habari.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa