Waziri wa Madini Mhe.Dkt.Doto Biteko amekemea utoroshwaji wa madini unaofanywa na baadhi ya wafanya biashara wasio waaminifu ambao bado hutorosha madini hayo.
Mhe. Biteko ameyasema hayo leo kwenye ziara ya kikazi Mkoani Geita katika eneo la Lwamgasa, Halmashauri ya Willaya ya Geita baada ya kutembelea Mgodi mdogo wa Nassoro Juma wa mwananchi, mialo miwili pamoja na mgodi wa mfano wa Lwamgasa wa serikali chini ya STAMICO
"serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Samia Suluhu Hassan imepunguza tozo mbalimbali kwa lengo la kuweka mazingira bora kwenye sekta ya madini"amesema Dkt. Biteko
Pia akatumia nafasi hiyo kutoa maelekezo mengine kwenye sekta anayoisimamia akisema.
“tayari tumewakamata watu 8 kwa tuhuma za utoroshaji madini, na nitoe onyo kwa mnaoendelea kwani mnatorosha madini kwa ajili ya nini wakati tayari serikali inayoongozwa na Mhe.Samia Suluhu Hassani ilikwisha kutengeneza mazingira mazuri kwa kupunguza tozo mbalimbali?” alisema Waziri Biteko
Pia amempongeza mchimbaji mdogo Nassoro Juma ambaye amekuwa akifanya kazi vizuri huku akiwa na mahusiano mazuri na wafanyakazi pamoja na jamii na ndiyo maana anachangia CSR,
Waziri Biteko alitoa agizo kwa maafisa madini wote nchini kuhakikisha wananchi kuacha kuweka mialo kwenye mnyumba zao na kuelekeza suala hilo lisimamiwe na serikali ya wilaya chini ya mkoa na kwamba kuanzia sasa yatengwe maeneo ambapo mialo yote itakaa hapo, itasajiliwa na wenye mialo nao wahakikishe wanaweka rekodi za dhahabu wanayoipata kwani imeonekana kwa kiasi kikubwa mapato yatokanayo na dhahabu inayotokana na Zebaki yameshuka kwa kiasi kikubwa kutokana na utoroshwaji wake. Vilevile aliiagiza STAMICO kuongeza ukubwa wa huduma baada ya mwitikio wa wateja kwani awali mgodi wa Lwamgasa uliwekwa kwa majaribio hivyo unazidiwa kwa sasa.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa geita Mhe.Rosemary Senyamule alisema anaipongeza Wizara ya Madini kwa kuutambua mkoa wa geita kuwa ni mkoa unaoongoza kwa uzalishaji wa madini ya dhahabu na kwamba dhamira iliyopo ni kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha Madini ya Dhahabu na ndiyo maana kwa kuanzia mkoa umejenga soko kubwa la Madini na unaendelea na jitizada kwa kushirikiana na wizara ili kuwasaidia wachimbaji wadogo ili waboreshe teknolojia ya uchimbaji.
Awali, Waziri Biteko alipata wasaa wa kusikiliza kero, maoni na pongezi kutoka kwa wananchi na wachimbaji wa Lwamgasa na kisha kuahidi kuchukua hatua mbalimbali katika utatuzi ya yale yaliyoonekana kuwa mahitaji ya wananchi hao ikiwamo kuomba kuruhusiwa kuchimba kwenye maeneo yaliyotolewa kwa vikundi na kushindwa kuyaendeleza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa