Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amewaagiza wataalam wa Wakala wa Barabara Tanzania( TANROADS) na Wakala wa Barabara za vijijini na mijini( TARURA) katika mkoa wa Geita kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi wa Mkoa huo juu ya matumizi sahihi na utunzaji wa barabara. Mhandisi Robert Gabriel ameyasema hayo wakati wa kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Geita kilichoketi tarehe 21/02/2019 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Mhandisi Gabriel ameongeza kuwa uwepo wa barabara nzuri katika Mkoa wake ni jambo la msingi na barabara ni moja ya raslimali adimu inayostahili matunzo hivyo wadau wa barabara wanatakiwa waendelee kuwaelimisha wananchi kutovamia hifadhi za barabara kwa kujenga, kulima, kupitisha mifugo, wizi wa alama za barabani, vyuma na makalavati. Pia kuepuka matumizi yote yasiyo rasmi na yasiyoruhusiwa.
Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa barabara ni uchumi na maendeleo kwani mazao, bidhaa mbalimbali za kibiashara husafirishwa kutoka eneo moja hadi jingine, zikitunzwa vizuri zinaondoa umaskini. Pia barabara imara inapokuwepo inasaidia kuokoa maisha ya wagonjwa na kina mama wajawazito kwa kuwawahisha katika vituo vya huduma za afya pindi inapohitajika.
Mkuu wa Mkoa wa Geita ametumia fursa hiyo pia kuwataka wataalam wa Wakala wa barabara kwa kushirikiana na wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Geita kufuatilia na kusimamia kwa karibu miradi inayotekelezwa ili kupata miradi yenye ubora wa hali ya juu na gharama ya miradi iendane na utekelezaji halisi.
“Mamlaka za barabara hakikisheni kazi za ujenzi na ukarabati wa barabara zinazotolewa kwa wakandarasi wawe ni wenye weledi, uadilifu, uzoefu na uwezo wa mitambo yenye ubora. Ni aibu kwa Mkoa wa Geita kumpa kazi ya ujenzi wa barabara aliyeharibu kazi katika mikoa mingine hivyo mnatakiwa kufanya utafiti wa kina kabla ya kuajiri mkandarasi yeyote.” Aliongeza Mhandisi Robert Gabriel.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania Mkoa wa Geita Mhandisi Harun Senkuku amesema kuwa licha ya jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha barabara zinatengenezwa bado wanakabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya dhamira mbaya ya baadhi ya wasafirishaji kupitisha mizigo mizito kwenye barabara kinyume na matakwa, sheria na kanuni za barabara.
Mratibu wa Wakala wa Barabara za vijijini na mijini( TARURA) wa Mkoa wa Geita Mhandisi Gaston Paschal amesema TARURA imejipanga kuwajengea uwezo wakandarasi wazawa ili waweze kufanya kazi zenye ufanisi. Pia kutoa elimu kwa wananchi kupitia mikutano ya watendaji wa Serikali na wanasiasa juu ya utunzaji wa barabara kwa mujibu wa sheria ya barabara yam waka 2007.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale ambaye ni mjumbe wa Bodi ya barabara ametoa ushauri kwa Wakala wa barabara vijijini na mijini( TARURA) kutenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya ukarabati wa barabara wa dharura pindi inapotokea barabara zimekatika hususani wakati wa kipindi cha masika.
Kwa Mwaka wa fedha 2018/2019 jumla ya shilingi Bilioni 3.28 za kitanzania zimetengwa kwa ajili ya miradi midogo ya maendeleo ya ukarabati wa barabara za Mkoa na Halmashauri za Wilaya katika Mkoa wa Geita
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa