Ni desemba14, 2022, siku ya pili tangu kuanza ziara ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi CCM mkoa wa Geita, ambapo halmashauri ya wilaya ya Geita imezikonga nyoyo za wajumbe hao pamoja na wananchi kufuatia ujenzi wa vyumba 347 vya sekondari vitakavyosaidia kupunguza msongamano madarasani na kuchochea ufaulu kwa wanafunzi, huku wananchi na viongozi kwa ujumla wakimshukuru rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia halmashauri hiyo shilingi bilioni sita na mililioni mia tisa arobaini (6,940,000,000) ili kuondokana na upungufu ambao ungesababisha wanafunzi wengi kushindwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022.
Hayo yamejili wakati wajumbe wa kamati hiyo walipotembelea miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu ya elimu na afya katika kata za Bugalama, Bugulula zilizopo jimbo la Geita na kata za Chigunga, Butundwe na Lwamgasa katika jimbo la Busanda huku msisitizo mkuu ukiwa ni kuwahimiza wazazi kuhakikisha wanafunzi wanafika shuleni, miundombinu inatunzwa, usafi unazingatiwa lakini pia kuongeza ufaulu.
Kiongozi wa msafara huo ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoka mkoa wa Geita ndg. Evarist Gervas amesema, ni wajibu wa viongozi kutangaza mazuri yaliyofanywa na serikali vilevile kuishukuru kwa yaliyofanyika Geita kiwemo suala la ujenzi wa madarasa bora na ya kisasa kama ambayo yamejengwa na kuing’arisha Geita DC, lakini pia kuhakikisha madarasa yaliyojengwa yanatunzwa.
“kwanza nimshukuru mhe.rais Samia Suluhu Hassan kwa makubwa yaliyotendeka kwakuwa isingelikuwa hivyo, leo tungelichangishana na wananchi na tusingelimaliza madarasa mengi hivi kwa pamoja. Lakini pia wazazi hakikisheni watoto wenu wanakuja shuleni wasiwe watoro, na walimu fundisheni ili madarasa haya yawe na matokeo kwakuwa ni mazuri sana. Tunzeni madarasa haya yakawe msaada leo, kesho na hata miaka mingi ijayo. Tuendelee kumuombea mhe.Rais lakini kutokana na usimamizi mzuri mliouonesha Geita DC, nami kwaniaba ya chama nachangia shilini laki tano (500,000) ili zisaidie ukamilishaji wa sehemu mlizokuwa mmeanza kujenga lakini pia viongozi wenzangu tuyaseme mazuri yanayotekelezwa na serikali yetu kwa kuitekeleza ilani ya CCM kwani wapotoshaji ni wengi” alisema MNEC Evarist.
Naye mkuu wa wilaya ya Geita mhe.Wilson Shimo ambaye pia katika ziara hiyo amemwakilisha mkuu wa mkoa wa Geita amesema “bado naendelea kutoa shukran kwa mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi alizotupatia Geita, hivyo wananchi sasa tutembee kifua mbele kwani hatuna vikwazo kwa watoto wetu kuanza kidato cha kwanza. Shime wazazi tuwapeleke na kuwahimiza watoto wetu kuja shuleni na kusoma wakati shule zitakapofunguliwa na mwisho tutegeme ufaulu kwani kwa miundombinu hii mizuri, mwanafunzi atakayeanzia kusomea humu sidhani kama atafeli”.
Kwa upande wake mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa na mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi mkoa wa Geita bw. Lucas Mazinzi ameonesha kufurahishwa na jinsi Geita DC ilivyomaliza madarasa mengi kwa wakati, huku akiomba kupewa mbinu ya ufanisi kisha kutoa zawadi ya mifuko kumi (10) ya saruji ili isaidie kukamilisha ujenzi wa miradi mingine ndani ya shule ya sekondari Isingilo Kata ya Lwamgasa
Katika hatua nyingine, mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya ya Geita bw. John Wanga ameeleza kuwa, pamoja na serikali kuipatia halmashauri hiyo zaidi ya bilioni 6 zitokanazo na fedha za Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19, pia halmashauri hiyo imepewa shilingi milioni mia moja themanini (180,000,000) kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matano (5) katika shule shikizi mbili (2) za Kawe na Nyamikoma pamoja na ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum kata ya Katoro hivyo kuishukuru serikali.
Wananchi nao hawakuwa nyuma kuipongeza serikali ambapo bi.Lucia Kanyamaiswa ambaye ni mzazi wa binti anayesoma katika shule ya sekondari ya serikali ya Isingilo kata ya Lwamgasa iliyopata vyumba kumi na nne (14) vya madarasa amesema ni muhimu kupongeza juhudi zilizofanywa na serikali kwakuwa isingelikuwa hivyo basi huu ungelikuwa wakati mgumu kwao kwa kuchangisha fedha ili wajenge vyumba vya madarasa na ni dhahiri ya kuwa wanafunzi wengi wasingejiunga.
Ziara hiyo imeshirikisha viongozi mbalimbali wa chama tawala na watendaji wa serikali na inatajiwa kuhitimishwa tarehe 15 januari 2022 katika halmashauri ya mji Geita
Geita ya Dhahabu, Utajiri na Heshima
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa