Halmashauri ya Wilaya ya Geita imepongezwa kwa kuanza mwaka mpya wa fedha Julai Mosi, 2019 ikiwa imetekeleza Ibara ya 57 ya Ilani ya Chama Tawala CCM ya mwaka 2015 kwa kutoa zaidi ya asilimia 100 ya lengo la asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwaajili ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia fedha inayotengwa kwaajili ya makundi ya Vijana, Wanawake na wenye Ulemavu katika ukumbi wa mikutano halmashauri ya wilaya ya geita.
Akitoa pongezi hizo, mgeni rasmi ambaye ni mkuu wa mkoa wa geita mhandisi Robert Gabriel amesema, anaipongeza halmashauri hiyo kwa kuvuka lengo la kuwezesha wananchi kiuchumi kwa kukabidhi vocha za jumla ya shilingi milioni mia moja ishirini na tatu Tshs.123,000,000 za robo ya nne ya mwaka wa fedha 2018/2019, huku akisisitiza vikundi hivyo kufuatiliwa ili vikue na kuwataka waliokopeshwa fedha hizo kurejesha kwa wakati.
“naipongeza sana halmashauri hii, viongozi wenye dhamana muendelee kujenga uaminifu uliopo, watendaji na SIDO msiwaache kundi hili bali endeleeni kuwaangalia kama daktari na mzazi wanavyofuatilia afya ya mtoto. Nanyi wananchi mliochukua mikopo hii, ni vyema muirudishe kwa wakati na wengine wakopeshwe. Mnapaswa kutambua kuwa, ni kupitia uongozi wa CCM uliyopo madarakani ndiyo maana fedha hizi zimewafikia kwani chama hiki kimejitofautisha na vingine kwa utendaji wake”, amesema mhandisi Gabriel.
Hakuishia hapo, mhandisi Gabriel amesema, ni kiu yake kuwa viongozi wataandaa siku maalum kwaajili ya kuona bidhaa zinazozalishwa na vikundi hivyo na kuwa sehemu ya soko kwa kuzinunua, vilevile ametumia fursa hiyo kuwaasa vijana kutotumia fedha hizo kuoa oa bali kuwekeza kwenye viwanda kama ilivyo adhima ya Serikali hii ya Awamu ya Tano.
Akisoma taarifa ya utoaji mikopo, Afisa Maendeleo wa Halmashauri Bi. Furaha Chiwile amesema, kwa mwaka wa fedha 2018/19 ilitengwa Jumla ya Tshs.331, 388,352 ambapo halmashauri imewezesha jumla ya Tshs.335, 000,000 sawa na asilimia 101 (101%) ya lengo kwa vikundi 59, wanawake vikundi 26, vijana vikundi 20 na wenye ulemavu vikundi 12. Pamoja na fedha hizo, wameweza kutoa Milioni Mia Moja Arobaini na Tisa (Tshs. 149,000,000) zilizorejeshwa kati ya zaidi ya Shilingi Milioni Mia Moja Sabini na Sita (Tshs. 176,719,000) kwa vikundi 21 vya wanawake na vikundi 6 vya vijana vyenye wanachama 585.
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Geita Mohamed Ally ameipongeza halmashauri hiyo na kusema hakuwahi kukutana na halmashauri inayowezesha wananchi kwa kiasi kikubwa kama ya geita na kwamba anafurahi kuona CCM imetimiza ahadi yake kwa asilimia zaidi ya iliyopangwa huku akiwakumbusha kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kupigia kura wakati utakapofika ili kupata nafasi ya kuendelea kuchagua viongozi sahihi wanaotimiza ahadi zao, huku Katibu wa UVCCM Geita Ally Rajab amewasihi kurudisha mkopo waliopewa kwa wakati.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ali Kidwaka ameseama, sasa wameamua kubadilika na kwamba kwa miaka mitatu nyuma hawakuweza kutoa kiwango kikubwa kama ilivyo leo, kikubwa amesisitiza juu ya urejeshwaji wa mikopo kwa wakati kwakuwa hadi sasa ni asilimia 52.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Elisha Lupuga amesema, kwa sasa wadhamini wa wakopaji wataanza kuwajibishwa endapo mikopo itachelewa kurejeshwa na kuwasihi wananchi kuendelea kuwapa wahe. Madiwani ushirikiano kwenye utekelezaji wa miradi kama ya elimu na afya .
Mwisho, baadhi ya wanakikundi Alex Bonoface na Benadetha Msendamila wakashukuru kwaniaba ya wenzao wakiahidi kwenda kuzalisha na kurejesha fedha hizo kwa wakati
Hafla hiyo ilihudhuliwa na wawakilishi wa kamati ya usalama wilaya, wawakilishi wa Bima ya Afya NHIF, Benki ya NBC, NSSF, Golden Line, SIDO na TRA n.k ambao wote kwa pamoja walipata nafasi ya kuelezea nini ambacho shirika au taasisi yake inakifanya ukihusianisha na wajasiriamali hao waliokopeshwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa