Ikiwa zimepita siku chache baada ya kufanyika mkutano wa wadau wa madini na vito vya thamani ulioongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Munngano wa Tanzania jijini Dar es Salaam na Wizara ya Madini, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa madini, hasa wauzaji na wanunuzi wa madini ya dhahabu kwa lengo la kuhakikisha soko la dhahabu linaanzishwa haraka iwezekenavyo.
Akiongea na wadau hao waliojitokeza kwa wingi katika ukumbi wa mikutano, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Gabriel amewaeleza wadau hao kuwa wanalo deni kubwa kufuatia ahadi waliyoitoa kwa Mhe. Rais Magufuli wakati wa kikao ikiwemo kutotorosha madini ya dhahabu na kuhakikisha serikali inapata mapato stahiki, hivyo kuona ni muhimu kuanzisha soko la dhahabu mapema iwezekanavyo wakati huu wa mpito.
Amesema “kwakuwa Geita ni Dhahabu, tunataka kufungua masoko ya uuzaji madini ya dhahabu haraka iwezekanavyo na mkurugenzi wa mji Geita tayari ametoa eneo kwenye soko jipya ili tuanze mara moja kwa soko la mkoa. Kutakua na Benki mbalimbali ikiwemo BOT na CRDB kwaajili ya kurahisisha shughuli nzima ya uuzaji dhahabu. Tutafanya biashara kwa mifumo ya kieletroniki, hakuna haja ya mtu kutembea na fedha nyingi, mambo ni kidijiti (digital), watakuwepo ofisi ya madini na ya mkurugenzi, lengo ni kwamba, mteja anamaliza kila kitu hapo hapo na ulinzi utaimarishwa hivyo ondoeni hofu”.
Mhandisi Gabriel amewaeleza ofisi ya madini mkoa kuwa, wanatakiwa kuyatambua maeneo ya ununuzi na wanunuzi wa dhahabu lakini pia kushauri vyema kuhusu usalama wa wanunuzi na kuhakikisha elimu ya namna ya kutumia mifumo ya kielektroniki kwa wanunuzi ili kuepuka kutembea na fedha nyingi mkononi kwa usalama wa maisha yao
Amewasihi wafanyabiashara na wadau wa dhahabu Geita kuwa, ulimwengu umebadilika na hawana haja sasa ya kuhatarisha usalama wao kwa kubeba fedha nyingi mkononi huku akiwasisitiza kutimiza ahadi ya kutokutorosha rasilimali madini ili kulinufaisha taifa, kisha akawaongoza wanunuzi na wauzaji hao hadi kwenye soko hilo ili kupanga ni namna gani wataweka ofisi zao ambapo wengi walionesha nia ya kuweka ofisi zao sokoni hapo.
Naye Bw. Christopher Kadeo ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Geita (GEREMA) amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa, watahakikisha deni walilonalo watalitimiza na kwamba wako tayari kutoa ushirikiano kwakuwa huu ni mwanzo mpya.
Kwa upande wake Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Geita Bw. Daniel Mapunda amesema, mkoa utakuwa na jumla ya vituo ama masoko tisa (9) yaa uuzwaji wa madini ya dhahabu ambapo kutakuwa na Soko Kuu la Mkoa Mjini Geita na masoko madogo madogo kwenye maeneo ya uzalishaji ambayo ni Lwamgasa, Nyarugusu, Katoro, Bwanga, Chato Mjini, Ushirombo, Masumbwe na Msalala.
Wakiwa eneo litakapokuwa soko la dhahabu, wadau hao wameonesha kuridhishwa na utaratibu uliopangwa kutumikia kisha wakajiorodhesha kwaajili ya kulipia maeneo zitakapokuwa ofisi zao, lengo la mkoa ikiwa ni kuwatambua wote wanajishughulisha na biashara ya madini ambapo awali waliotambulika ni wale wenye viwanda vya uchenjuaji na uchakataji dhahabu (elutions)
Pamoja na hayo, wadau hao wameahidiwa kuwa na vikao endelevu ili kupata mawazo yao kuhusu namna bora ya kuendesha shughuli zao huku wakimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa jitihada na kuwashirikisha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa