Mkuu wa Mkoa wa Geita na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa Mhe. Eng Robert Gabriel, ameongoza operesheni maalum kwa wafanyabiashara katika eneo la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro Januari tatu, 2019, Halmashauri ya Wilaya ya Geita, yenye lengo la kuhakikisha kuwa hakuna mfanyabishara anayeingiza biashara za magendo, haramu na zile zisizo na alama za uthibiti ubora kama TBS na TFDA ikiwa ni jitihada za kuhakikisha wananchi wanakuwa salama lakini pia Serikali inapata kodi zake stahiki.
Mhe. Eng. Gabriel amewataka wafanyabishara kutambua kuwa, wanao wajibu wa kufuata sheria, kanuni na taratibu wanapoamua kuingia kwenye biashara baada ya kukuta baadhi ya wafanyabiashara wakiuza bidhaa zaidi ya zile walizozisajili, huku akihimiza maafisa wa TRA kuendelea kutekeleza zoezi hilo kwa wafanyabiashara wote ili kuwabaini na kuwachukulia hatua wote wanaokwepa kodi ndani ya Mkoa.
Amesema, “leo tumeona maeneo 14 tu, tunafanya operesheni hii kujiridhisha kama bidhaa zinapotoka panatambulika, zina risiti, pia zimethibitishwa na kama serikali inapata mapato. Inasikitisha kuona mtu anasema anauza hiki kwenye leseni, wakati ana zaidi ya anavyoviuza. Hivyobasi, TRA fanyeni kazi ya ziada kujua kama bidhaa hizi zimeletwa ni kwaajili ya kuuzwa hapa au nje ya nchi”. Alisisitiza.
Wakati huo huo Eng. Gabriel, ameongea na wananchi waliokuwa jirani na biashara hizo, akiwaeleza kuwa operesheni hiyo imekuja na haitaruka duka, hivyo ni vyema kuzingatia matakwa ya sheria kwani ni kupitia kodi hizo, serikali imeweza kuboresha miundombinu ya elimu, afya, maji, barabara n.k
Katika operesheni hiyo, baadhi ya wafanyabishara wameombwa kutoa ushirikiano kwa maafisa wa TRA wanapoendelea kufanya kaguzi na kuwa tayari kupewa maelekezo na kuyafuata ikiwemo ya ulipaji wa faini, kusajili biashara zao kuendana na leseni, lakini pia kuepuka udanganyifu.
Mmoja wa wafanyabiashara (jina limehifadhiwa) amekutwa ana leseni ya uuzaji wa vilainishi vya mashine (lubricants) wakati anazo bidhaa nyingi za matairi na mashine, huku mwingine akikutwa na pombe iitwayo Ndume ambayo bado haijathibitishwa kama ni salama kwa watumiaji (haina nembo ya TBS), ambapo imeelekezwa kwamba, TFDA Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Kanda wafike mapema ili kutolea suala hilo ufafanuzi kwani pamoja na kuwa na cheti kutoka TFDA, bado kilitiliwa shaka na Bw. Gasper Moshy ambaye ni Mratibu wa TFDA Halmashauri ya Mji Geita kuwa huenda ni cha kughushi.
Kwa upande wao maofisa wa TRA wakiongozwa na Meneja wa Mkoa Bw. James Jilala wamemhaidi Mkuu wa Mkoa kuwa, wanaendelea kutoa elimu na watatekeleza maelekezo aliyoyatoa na kuhakikisha taarifa inafika kwake kwa wakati juu ya namna watakavyoendelea kushughulikia wakwepa kodi ikiambatana na hatua walizochukuliwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa