Mkoa wa Geita umekua miongoni mwa mikoa vinara mitatu iliyoongoza nchi nzima katika ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Hayo yamebainishwa na Mhe. Seleman Jafo (Mb), Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI alipokuwa akisoma Taarifa ya Hali ya Ukusanyaji wa Mapato Katika Mamlaka za Serikali za Mitaa katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Jijini Dodoma tarehe 05.10.2018 iliyoonesha kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zimekusanya Kiasi cha Shilingi 553,390,075,912/= kati ya shilingi 687,306,661,000/= sawa na asilimia 81 ya lengo.
Waziri Jafo ameanza kwa kusema, “tulizoea kutajiwa shule na wanafunzi waliofanya vizuri na vibaya kwa mitihani ya darasa la saba, kidato cha nne cha sita, lakini sasa tumeona ni vyema tuujulishe umma wa Watanzania kuwa Halmashauri zetu zimekusanya kwa kiwango gani mapato yatakayowezesha huduma kurudi kwenye jamii, na hili litakuwa fundisho kwa wasiofanya vizuri”.
Mhe. Jafo amezitaja Halmashauri zilizoongoza katika makusanyo akiitaja Halmashauri ya Mji Geita kama Halmashauri iliyoongoza kwa ujumla kitaifa kwa kukusanya Shilingi 6,863,169,216/= kati ya lengo la kukusanya shilingi 3,150,910,000/=sawa na asilimia 218
Kwa upande mwingine, Mhe. Jafo ameutaja Mkoa wa Geita kama Mkoa wa Pili Kitaifa kwa kukusanya mapato yake kwa kufikia asilimia 104, hii ikiwa na tafsiri kuwa, Halmashauri 6 za Mkoa wa Geita zimepelekea matokeo mazuri kimkoa.
Amemaliza taarifa yake kwa kutoa maagizo kuwa, asilimia 81 iliyopatikana kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ndiyo kitakua ni kipimo na kwamba mapato ya Halamshauri zote nchini kwa mwaka wa fedha 2018/2019 yasishuke chini ya asilimia 81 na kwamba kitakuwa ni kipimo cha Mkurugenzi wa Halmashauri kuona kama anastahili kubaki kwenye nafasi hiyo.
Kufuatia taarifa hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel ameipongeza Halmashauri ya Mji Geita Kwa Kushika nafasi ya kwanza Nchi nzima na vilevile kupongeza juhudi zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na Halmashauri za Mkoa wa Geita katika kukusanya mapato.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa