Katika kuhakikisha migogoro ya ardhi inapungua nchini, utambuzi wa mipaka ni moja ya jitihada ambayo imekuwa ikifanywa na serikali katika maeneo mbalimbali hasa pale inapotangaza maeneo mapya ya utawala ambayo kwayo ni lazima kuwepo na ufahamu wa pamoja wa mipaka ya maeneo husika ili kuepukana na migogoro mingi ya ardhi ambayo imekua ikijitokeza. Jambo hili linapelekea uwepo wa kikao baina ya Makatibu Tawala na Wataalamu wa Mikoa wa Kagera na Geita kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Kagera tarehe 08.02.2019.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa kikao kilichowashirikisha Makatibu Tawala Mkoa wa Kagera na Geita pamoja na wataalam wa Sekta ya Ardhi kutoka Sekretarieti za mikoa hii, Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Prof. Faustin Kamuzora amesema amepokea zoezi hilo na kwamba zoezi hilo litakavyofanyika kama ilivyotarajiwa.
Amesema “nishukuru tu kwa uwepo wa zoezi hili zuri na tumelipokea hivyo naamini litafanyika kama ilivyoelekezwa na ninaamini litapunguza migogoro, hivyo ni vyema tukapitishana kwenye ramani kuona mahali tunapopafanyia kazi kwa uelewa zaidi”
Akiongea baada ya ufunguzi wa kikao hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Bw. Denis Bandisa ameeleza kuwa, maeneo mapya yanapoanzishwa mipaka na ramani hutayarishwa, jukumu linalotekelezwa na mkoa mama na mkoa mpya ambapo Mkoa wa Geita umetokana na Mikoa ya Mwanza, Kagera na Shinyanga jambo linalopelekea sasa kujiridhisha na kwenye ramani.
Bw. Bandisa ameendelea kusema kuwa, kwa mikoa ya Mwanza na Shinyanga hakuna changamoto isipokuwa upande wa Kagera (upande wa Biharamuro) na Geita (kwa upande wa Bukombe) ambapo awali iliripotiwa kuwepo kwa mgogoro wa mpaka baina ya pande hizi. Hivyo utekelezaji wa zoezi hili la utambuzi wa mipaka unaenda sanjari na kumaliza mgogoro huo wa muda mrefu na utawashirikisha wataalamu wa Ardhi kutoka Sekretarieti za Mikoa ya Kagera na Geita, pamoja na wa Halmashauri za Biharamuro na Bukombe.
Amesema, “zoezi la sasa ni kuweka mipaka ya ardhi kikamilifu na itambulike na mamlaka zote za mikoa hii, jambo ambalo ni njia mojawapo ya kuepuka migogoro. Kwa maana hiyo, wataalamu sasa wanakwenda kujiridhisha na kuweka hizo alama na mwisho taarifa ya kitaalamu kuwasilishwa ili viongozi waweze baadaye kuzijulisha jamii juu ya mipaka hiyo”.
Kwa upande wake Bw. Charles Saguda ambaye ni Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Miundombinu kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Geita amesema, zoezi hili limetokana na maelekezo mahsusi ya kufanya utambuzi na kuweka alama za kudumu katika mipaka ya Mkoa, Wilaya, Tarafa, Kata, Kijiji/Mtaa na Kitongoji yaliyotolewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Hivyobasi Mkoa wa Geita umeanza utekelezaji wa maelekezo hayo katika mpaka wa Mikoa ya Geita na Kagera kisha kuwapitisha wajumbe kwenye ramani inayoonesha mipaka ya mikoa hii.
Makatibu Tawala wa Mikoa hii wameazimia kazi kazi hii kuanza mapema tarehe 15 Februari 2019.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa