Ni majira ya saa nne asubuhi ya tarehe 20.01.2019, ujumbe wa Bi.Natalie BOUCLY, Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Tanzania unawasili na kupokelewa Mkoani Geita na mwenyeji wao Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Geita kisha kufanya mazungumzo yenye lengo kuu la ushirikiano katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji.
Akiukaribisha ujumbe huo, Mhe. Mhandisi Gabriel amemweleza Bi. Natalie juu ya namna ambavyo mkoa umejipanga kuwa na Geita mpya huku akiitaja miradi ya kimkakati itakayotekelezwa kwa mwaka huu 2019, itakayobadili taswira ya mkoa na kuufanya uwe wa kiuwekezaji na kuinuka kiuchumi.
Amesema, “Geita tunahitaji matokeo kwenye miradi, tungependa tuungane nanyi UNDP katika kuhakikisha tunafungua ukanda wa uwekezaji na utalii Geita, tuwe na kijiji cha utalii, lakini vilevile tuwe na utalii wa asili, tuwakaribishe wageni kujifunza mila na desturi (tamaduni) za jamii ya Geita. Jambo jingine ni kuandaa soko maalumu kwaajili ya wachimbaji wadogo wadogo kuweza kuuza dhahabu yao huku wakipata teknolojia bora ya uchakataji na uchenjuaji madini hayo bila kusahau kuitangaza Rubondo kama hifadhi inayopatikana Geita yenye vivutio vingi”.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Tanzania Bi. Natalie BOUCLY aliyeambatana na Bw. Amon Manyama, Mratibu wa Miradi UNDP na Bw. Joshua Mirumbe ambaye ni Mshauri, alionesha kufurahishwa na mapokezi aliyoyapata kutoka kwa mwenyeji wake huku akisema “nimefurahi sana, sijasemeshwa Kifaransa tangu nimekuwa nikizunguka” kisha kueleza jinsi UNDP inavyofanya kazi zake nchini ikiwemo uhifadhi wa misitu asilia.
Bi Natalie amesema, “kwa Geita tutaangalia namna ya kushirikisha Kampuni ya Africa Mining Vision na UNDP Ghana ili kuweza kufanikisha suala la namna nzuri ya kusaidia soko la dhahabu ya wachimbaji wadogo wadogo Geita, kwakuwa tunao wataalam katika eneo hili, lakini vilevile kupitia mradi tunaoendelea nao wa utunzaji misitu asilia, tutaweza kuitangaza Hifadhi ya Rubondo, na tunawapongeza kwa utajiri uliyopo Geita, Geita ni Dhahabu”.
Katika mazungumzo hayo, Bi. Natalie aliongeza kusema kuwa, ni vyema kushirikisha nchi jirani zenye shughuli za kitalii ili katika safari zao, Geita iwe ni sehemu ya utalii kwani watalii wengi hupenda hata kuangalia mashamba ya mazao kama yanayopatikana Geita ikiwemo Nanasi, Pamba, Muhogo, uchimaji mdogo mdogo na hatua za upatikanaji wa dhahabu n.k na kwamba hata katika mikutano watakayokuwa wakiendesha wanapokuwa na wafadhili mbalimbali, basi watakuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Geita na vivutio vyake ikiwemo Kisiwa cha Rubondo.
UNDP Tanzania kupitia uwakilishi wake, wamesema wataendelea kuwa na ushirikiano na Geita katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, hivyo wafurahia uwepo wao Mkoani Geita kutokana na namna mkoa ulivyojipanga kuinua maisha ya wananchi wake.
Miongoni mwa waliyoshiriki katika mazungumzo hayo ni Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Josephat Maganga, Mkurugenzi wa Mji Geita Eng. Modest Aporinary na Meneja wa SIDO Mkoa wa Geita Bw. Japhary Donge.
Kwa hakika, Geita mpya inakuja kutokana na ndoto na maono mengi aliyonayo Mkuu wa Mkoa Mhandisi Gabriel, na katika mikutano yake amekuwa akimwomba Mungu ili mazuri mengi anayoyapanga kwaajili ya Geita yatimie na mara nyingi amekuwa akisema “tulichelewa sana, Geita ni tajiri, hivyo ni lazima mkoa ufanane na utajiri ulionao, wananchi pia wanufaike na utajiri wa mkoa huu”.
Hivyobasi, Watanzania mnaendelea kukaribishwa mkoani humu, mkoa wa kiuwekezaji, hakuna urasimu, rushwa wala ubadhilifu “kwetu ni zilipendwa”, mazingira sahihi na rafiki kwa uwekezaji.
Geita: Amani, Umoja na Kazi
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa