Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama ya Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita wameipongeza Halmashauri ya Mji Geita Kufuatia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu, afya na barabara kwa kutumia mapato ya ndani.
Pongezi hizo zimetolewa leo desemba 15, 2022 wakati wajumbe wa kamati hiyo wakihitimisha ziara yao kutembelea na kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ile ya Fedha za Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 huku msisitizo mkuu ukiwa ni utunzaji miundombinu hiyo, uhamasishaji watoto kuhudhuria shule zitakapofunguliwa, kupanda miti ili kutunza mazingira, kuuthamini mchango wa wananchi, lakini pia kuhakikisha viongozi wanawasaidia wananchi kujua fedha zilizoletwa na serikali na matumizi yake ili kuwadhibiti wazushi na wapotoshaji.
Akiongea katika maeneo tofauti walipotembelea wajumbe wa kamati hiyo, hususan akiwa katika Shule ya Msingi Kabuyombo yenye wanafunzi mia nane (800), kiongozi wa msafara ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kutoka mkoa wa Geita bw.Evarist Gervas amesema, " niwapongeze Geita Mji kwa namna ambavyo mmejitahidi kutumia mapato ya ndani kujenga madarasa kwa sehemu nyingi tulizozipitia siku ya leo, lakini hata kutumia fedha za wajibu wa kampuni kwa jamii yaani CSR. Ombi langu, tuendelee kuitunza miundombinu hii, tuongeze kasi ya ujenzi vituo vya afya lakini pia kuwahamasisha wanafunzi kuja shuleni pindi zitakapofunguliwa”
“hatuwezi vilevile kusahau kupongeza jitihada za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa fedha tulizozipokea Geita, tumuunge mkono mhe. Rais na viongozi tuisaidie jamii ijue kutofautisha matumizi ya fedha zitokanazo na tozo na hizi zitokanazo na mapambano dhidi ya UVIKO-19 ili kuwadhibiti wapotoshaji na naomba niwaahidi wanakabuyombo, nitatoa mabati, mbao za kupaulia na gharama za upauaji ikiwa mtaongeza vyumba vingine kwa vifaa vya ujenzi vilivyobakia kwenye ujenzi huu, lakini pia naomba kumkabidhi shilingi elfu hamsini (50,000) mkuu wa shule ya sekondari wasichana Nyakumbu bi.Georgia Mugashe kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa madarasa pamoja na matokeo mazuri kwa kidato cha nne, hongera sana" aliongeza MNEC Evarist.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita bibi. Alexandrina Katabi naye hakusita kusisitiza juu ya ushirikiano ikiwa Chama na Serikali hujenga kwa pamoja hivyo ni vyema kuendelea kuweka nguvu za pamoja katika usimamizi wa miradi, kisha kuwaasa Halmashauri ya mji kuzingatia kupeleka wataalam kusimamia miradi hata pale wanapowapatia wananchi fedha za miradi, yaani wasiwaache peke yao na kutekeleza ujenzi wa miradi, jambo linalofanya itofautiane katika ubora kati ya ile inayojengwa na wananchi na ile inayoletewa fedha na serikali.
Katika hatua nyingine, mkuu wa wilaya ya Geita mhe. Wilson Shimo ambaye katika ziara hiyo amemwakilisha mkuu wa mkoa wa Geita, ameishukuru kamati hiyo na kuahidi kutekeleza maagizo na ushauri uliotolewa kwao huku akiendelea kuipongeza Halmashauri ya mji Geita kwa utekelezaji wa miradi mingi kwa mapato ya ndani na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi alizozitoa ili kuikwamua jamii kubwa ya watoto wa Geita ili wasome.
Akihitimisha ziara hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita Bw. Lucas Mazinzi kama ilivyo ada amewashukuru Geita Mji kwa mapokezi mazuri na ameendelea kusisitiza juu ya kuthamini mchango wa wananchi kwenye ujenzi wa miradi, akihimiza ushirikishwaji wananchi lakini vilevile kuhakikisha miradi inamalizika kwa wakati bila kupoteza muda mwingi.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa madarasa mawili shule ya msingi Kabuyombo kwa shilingi milioni ishirini na tisa, laki tisa themanini na tano elfu (29,985,000.00), ujenzi wa madarasa mawili shule ya msingi Nguzo Mbili kwa shilingi milioni ishirini na tisa, laki saba thelathini na sita elfu (29,736,000), ujenzi wa bwalo shule ya sekondari Mwatulole kwa shilingi milioni mia moja hamsini na tatu, laki nane arobaini na tisa elfu mia sita thelathini (153,849,630), ujenzi wa kituo cha afya Bulela kwa shilingi milioni mia nne (400,000,000), ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami nyepesi ya Mwanza Junction-Jengo la Utawala GTC-Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Nyumba za Askari-Chuo cha VETA yenye urefu wa Km.1.3 awamu ya pili kwa shilingi milioni mia tisa hamsini na sita, laki nane na tisini na sita elfu (956,896,000), Ujenzi wa Vyumba viwili vya madarasa sekondari ya wasichana Nyankumbu kwa shilingi milioni arobaini (40,000,000) yote kwa ujumla ikiwa na thamani ya shilingi bilioni moja, milioni mia sita na kumi, laki nne sitini na sita na mia sita thelathini (1,610,466,630)
Zaiara hiyo imehusisha viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa na Wilaya, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, wataalam kutoka ofisi ya mkugenzi wa mji Geita pamoja na wataalam kutoka TARURA na GEUWASA
Geita ya Dhahabu, Utajiri na Heshima
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa