Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Ndugu Mohamed Gombati ametoa pongezi za dhati kwa timu zote zilizofanikisha Mkoa wa Geita kuingia katika nafasi kumi bora za juu kitaifa katika Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi na Sekondari Tanzania ambayo yalihitimishwa katika ngazi ya kitaifa hivi karibuni huko mkoani Tabora.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii hivi karibuni, Katibu Tawala Mkoa wa Geita amesema kuwa wanajivunia jitihada kubwa zilizofanywa na vijana hao ambao kupitia ushindi walioupata wameutangaza vyema Mkoa wa Geita kupitia michezo ambapo ana imani kuwa wadau mbalimbali wa michezo watautembelea Mkoa wa Geita kwa lengo la kuangalia vijana wenye vipaji na kuviendeleza.
Afisa Elimu Mkoa wa Geita Mwalimu Anton Mtweve ameeleza kuwa Mkoa wa Geita umepata nafasi ya sita kitaifa katika mashindano ya UMITASHUMTA na kwa upande wa mashindano ya shule za Sekondari UMISSETA Mkoa ulipata ushindi wa nafasi ya saba. Mkoa wa Geita umefanikiwa pia kutoa wachezaji tisa watakaojiunga na timu ya Taifa ya mpira wa mikono pamoja na vijana wanane ambao watajiunga na Timu za vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 katika Timu za Simba, Azam na KMC.
Mwalimu Mtweve ameongeza kuwa makombe yaliyopatikana kwa upande wa mashindano ya UMITASHUMTA ni mshindi wa pili Mpira wa mikono wasichana (Handball), mshindi wa tatu soka kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, mashindi wa tatu mpira wa pete wasichana (Netball), mshindi wa tatu mpira wa kikapu (Basketball) na kupata medali 14 ikiwa tatu ni za dhahabu na kumi na moja za fedha kwa upande wa riadha.
Afisa Elimu Mkoa amesema katika mashindano ya UMISSETA Mkoa wa Geita uliibuka na kombe la mshindi wa kwanza mpira wa miguu wavulana(Football), Kombe la mshindi wa kwanza mpira wa pete wasichana( Netball), Kombe la mshindi wa pili mpira wa mikono wasichana( Handball) na medali sita ikiwa tatu ni za dhahabu na tatu za fedha katika mchezo wa riadha.
Akizungumzia masuala yaliyochangia kuwapatia mafanikio hayo, Mwalimu Mtweve amebainisha kuwa morali ya juu waliyokuwa nayo wachezaji wote pamoja na ushirikiano kati ya wanafunzi, walimu na viongozi ni miongoni mwa sababu kubwa iliyowafanya wafanikiwe kwa kiwango kikubwa kwani kila mmoja alikusudia kulenga kupata ushindi katika mashindano hayo.
Mwalimu Mtweve ametoa rai kwa wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Geita wakishirikiana na wataalam wa Idara za Elimu pamoja na Vitengo vya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuanzisha kambi maalum( vitalu vya michezo) mbalimbali kwa kila Halmashauri ili kutengeneza timu imara zitakazofanya vizuri Zaidi katika Mashindano yajayo
Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA yalianzishwa kwa lengo la kuinua vipaji na kuviendeleza pamoja na kuwakutanisha wanafunzi kutoka katika mikoa yote ili kuwajengea uzalendo na kufahamiana miongoni mwao.
Mashindano hayo yanaandaliwa na kusimamiwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo kwa mwaka huu yalibebwa na Kauli Mbiu isemayo “Tunajivunia mafanikio katika sekta ya elimu, michezo na Sanaa, Hima Mtanzania shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa