Kama ilivyo kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Na.292 Marekebisho ya Mwaka 2015 Kifungu cha 9(5), ambacho kinamtaka kila Msimamizi wa Uchaguzi na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kuapa viapo vya Uaminifu, Utii na Uadilifu Mbele ya Hakimu baada ya kuteuliwa, mkoa wa Geita umetekeleza sheria hiyo kwa kuwaapisha jumla ya wasimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa sita (6) kutoka halmashauri sita za zinazounda mkoa huu walioambatana na maafisa uchaguzi kutoka kwenye halmashauri hizo.
Akizungumza ofisini kwake kabla ya tukio la kuapishwa wateule hao lililofanyika Septemba 12, 2019, Katibu Tawala Mkoa wa Geita Bw. Denis Bandisa amesema, wasimamizi wa uchaguzi walioteuliwa wanapaswa kuzingatia kuwa uchaguzi kwa mwaka huu umepangwa kufanyika Novemba 24, 2019 na hivyo wanapaswa kutambua yakuwa, kiapo walichokula ndicho kitawafanya wafanye kazi hiyo vizuri na watawajibika kwacho iwapo hawatafanya vizuri.
“pamoja na kutambua wajibu wenu kupitia kiapo mlichokula, ambacho kimewapa uhalali wa kufanya majukumu yenu yakiwemo ya kutoa tangazo la majina ya vijiji, mitaa na vitongoji kwa wakazi wa maeneo hayo kwa kuzingatia orodha ya vijiji, vitongoji na mitaa kama ambavyo yametolewa kwenye tangazo la serikali, mnatakiwa kuhakikisha kesho mnatangaza maeneo haya ya uchaguzi ikiwa ni jukumu lenu la kwanza kulitekeleza, hivyo ninaamini mtatekeleza majukumu yenu kwa haki na uadilifu”, amesema Bandisa.
Bw. Bandisa amemaliza kwa kuwasisitiza wasimamizi hao wa uchaguzi akiwaambia kuwa wanatakiwa kutambua kwamba, wao ndiyo watakuwa wasemaji wa kutoa maelezo na maelekezo mbalimbali kuhusiana na uchaguzi utakaofanyika, lakini pia wataunganisha ratiba za kampeni kutoka kwa vyama mbalimbali vya siasa kwa kushirikiana na mkuu wa polisi wilaya (OCD) ili kuepusha migongano na miingiliano wakati wa kampeni na mwisho kuunganisha taarifa ya matokeo ya uchaguzi na kuweka kumbukumbu.
Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Geita Mhe.Gabriel Nimrod Kurwijila kabla ya kuwaapisha walioteuliwa amewaambia kuwa, wanapaswa kutambua yakwamba, kwa sasa wanaajiriwa kwa kazi ya kusimamia uchaguzi kutoka kwa mwajiri wao ambaye ni waziri mwenye dhamana na uchaguzi wa serikali za mitaa, hivyo kazi hiyo ikafanyike kwa kadiri ya viapo watakavyoapa, kisha kuwaapisha tayari kwa kuanza kazi.
Kwa upande wake Bi.Sania Mwangakala ambaye ni Mratibu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Geita, amewapongeza wasimamizi hao kwa kuteuliwa na kusema lengo la kukutana hapo ni wao kuapa ili kuwa huru kuanza kutekeleza majukumu yao.
Jumla ya Mitaa 65, Vijiji 486 na Vitongoji 2,195 vitashiriki katika wa Serikali za Mitaa Novemba 24, 2019
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa