Shule ya Sekondari Geita imeshika nafasi ya kwanza kwa upande wa Shule za Serikali Kanda ya Ziwa katika matokeo ya mtihani wa utamilfu( Mock) kidato cha nne 2025.
Akitangaza matokeo hayo tarehe 16 Agosti 2025 katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya wasichana Nyankumbu Geita mjini, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Geita Dkt. Elfas Msenya amemtaja mwanafunzi Alex Theojenes James wa Shule ya Sekondari Geita aliyeongoza kundi la wavulana wenye ufaulu bora kwa kupata Divisheni 1.7
Dkt. Msenya ameeleza kuwa Mkoa wa Mwanza umeongoza katika matokeo ya jumla ya Mtihani wa Utamilifu (MOCK) kwa kidato cha nne kanda ya ziwa mwaka 2025 baada ya kupata ufaulu wa jumla wa asilimia 94.11 kwa shule zote.
Mtihani wa MOCK kidato cha nne kanda ya ziwa ulijumuisha mikoa sita ambayo ni Geita, Kagera, Mara, Mwanza, SImiyu na Shinyaga na ulifanyika kuanzia Julai 14, 2025 na kumalizika Agosti 01, 2025.
"Simiyu imeshika nafasi ya pili kwa asilimia 91.31, nafasi ya tatu ni Shinyanga kwa asilimia 89.71, Kagera nafasi ya nne asilimia 84.35, Geita nafasi ya tano asilimia 83.58 na Mara nafasi ya sita asilimia 80.58", ameongeza Dkt. Msenya.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Geita ameeleza kuwa mtihani ulihusisha shule 1,401 kati yake shule 1,115 za Serikali na shule binafsi 246 kutoka Halmashauri zote 43 pamoja na watahiniwa 151,649, wakiwemo wavulana 74,142 na wasichana 74,424.
Dkt. Msenya amefafanua kuwa dhamira kuu ya mtihani huo ni kupima uwezo wa wanafunzi kitaaluma, kupima ufundishaji wa walimu kwa mwaka 2025 iwapo wamefikia malengo ya kitaaluma na kupima ujuzi wa wanafunzi shuleni.
Dkt. Msenya ameagiza tathimini ya ifanyike kwa kina kwa ngazi zote ambazo ni mkoa, halmashauri na shule na mapungufu yatakayobainika yafanyiwe kazi na masahihisho yafanyike kati ya Agosti 15 hadi 25, 2025 ili kuwezesha wanafunzi walioshindwa kufanya mtihani wa Mock waweze kufanya mtihani wa Taifa wa kuhitimu kidato cha Nne.
Akiwasilisha taarifa ya matokeo hayo ,Mwenyekiti wa Maofisa Elimu Tanzania, Martin Nkwabi amefafanua kuwa ni watahiniwa 145,318 pekee kati yao wavulana 70,894 na wasichana 74,424 sawa na asilimia 95,83 walifanya mtihani.
"Watahiniwa 6,331 kati yao wavulana wakiwa 3,248 na wasichana 3,083 sawa na asilimia 4,17 hawakufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali hasa zaidi ikiwa ni utoro", amesema Nkwambi.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Geita Mwl. Ally Dauda amesema siri kubwa ya wanafunzi wake na shule kiujumla kufanya vizuri katika mtihani huo ni ushirikiano uliopo baina ya walimu, wazazi/ walezi na wanafunzi, kutenga muda wa ziada wa kufundisha wanafunzi, kuwapa wanafunzi majaribio na mitihani mara kwa mara kwa lengo la kuwapima kitaaluma pamoja na kusimamia vyema nidhamu ya wanafunzi.
Katika matokeo hayo, Mkoa wa Geita umefanikiwa kupata wanafunzi watatu walioingia kumi bora ambao wanatoka katika Shule za Sekondari Geita na Wasichana Nyankumbu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa