Kwa mara nyingine tena, Geita inaingia kwenye historia ya kupata zaidi ya Bilioni 9 kutoka Mgodi wa Dhahabu Geita GGML, fedha za wajibu wa kampuni kwa jamii (CSR) kwa kutia saini hati ya makubaliano baina yake na halmashauri mbili za Wilaya na Mji Geita Agosti 16, 2019 katika ukumbi wa mikutano ofisi ya mkuu wa mkoa wa geita.
Akishuhudia utiaji saini hati ya makubaliano hayo, mkuu wa mkoa wa geita mhandisi Robert Gabriel, ameupongeza mgodi huo kwa kuwa wa kipekee kuendelea kutekeleza takwa hilo la kisheria kupitia utaratibu wake iliyojiwekea wa kutoa asilimia 0.7 ya mapato ghafi inayopata kwa kila mwaka, huku pia akiupongeza uongozi wa wilaya na halmashauri za wilaya na mji geita kwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya CSR kwa mwaka 2018.
“pongezi kwenu GGML, pongezi halmashauri za wilaya na mji geita kwani fedha hizi zitakwenda kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo kwa halmshauri ya wilaya kujenga soko la kisasa katoro, mnada wa kisasa, miradi ya mazingira, umaliziaji miradi viporo pamoja na uimarishaji sekta za elimu na afya. Kwa halmshauri ya mji geita, hongereni kwa kuweka mpango wa ujenzi wa uwanja wa mpira, utengenezaji miundombinu kwenye eneo la uwekezaji (EPZA), uboreshaji miundombinu ya elimu na afya vilevile utekelezaji wa agizo la mhe.Rais Magufuli la kutenga fedha kujenga barabara ya lami kutoka njia kuu kupitia nyumba za askari (kambi ya Sirro) hadi hospitali ya mkoa inapojengwa”, alisema Mhandisi Gabriel.
Kipekee mkuu wa mkoa amezipongeza timu za CSR zenye watendaji wa mgodi huo na wa serikali na kuutaka Mgodi wa GGML kuwa na mpango kazi wa utekelezaji wa miradi hiyo na kwamba anaamini ujenzi wa nguvu kazi yaani force account utatumika na taratibu za manunuzi kuzingatiwa.
Mhandisi Gabriel amemaliza kwa kumweleza mkurugenzi mkuu wa GGML kuhakikisha anaisaidia serikali kutambua makampuni yanayotoa huduma katika mgodi huo na kwamba waeleweshwe vyema juu ya uwajibikaji wao kwa jamii huku waandishi wa habari wakiaswa kuendelea kuyatangaza mema na mazuri yanayofanyika mkoani hapa
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa mgodi wa GGML Richard Jordinson amesema, kama mgodi wanajivunia mafanikio haya makubwa wakiamini katika kufanya kazi pamoja na jamii inayowazunguka ili kuwe na uwajibikaji wa pamoja katika kutekeleza na kuitunza miradi ya maendeleo inayoidhinishwa kupitia mchakato shirikishi unaosaidia kupata miradi endelevu yenye tija kwa jamii inayowazunguka.
Bw.Jordinson amemaliza kwa kusema kuwa, GGML inaendelea kuunga mkono serikali ya Tanzania kutekeleza miradi endelevu katika maeneo ya kimkakati yaliyoainishwa na Mpango wa Serikali wa Miaka Mitano, Dira ya Maendeleo ya 2025 na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030. Vilevile mgodi huu utaendelea kushirikiana na halmashauri na jamii ya Geita katika kuanzisha na kusimamia miradi muhimu ambayo itasaidia kujenga mustakabali mzuri kwa jamii husika.
Mwinyikheri Baraza kwaniaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa ameipongeza GGML na kuwaasa viongozi kuendelea kutangaza mazuri yatokanayo na miradi ya CSR akisema kama chama wanatoa Baraka zote akiomba ushirikiano uendelee ili miradi hiyo itoe matokeo chanya.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita Leonard Bugomola ametumia wasaa huo kushauri hatua ya utiaji saini kufanyika mapema ikiwa hatua ya leo imebakiza miezi minne kumaliza mwaka ikiwa fedha za mwaka huu 2019 bado hazijatumika ingawa wapo tayari kuanza kazi jumatatu ya Agosti 19, 2019, huku Mwenyekiti Halmashauri ya Wilaya ya Geita Haraka Lupuga akiendelea kushukuru kwa jinsi mgodi ambavyo umekuwa msaada kwa jamii ya geita akiomba wasichoke kusaidia inapobidi na kuomba kuharakishwa kwa vifaa vya ujenzi wakati kazi itakapoanza.
Akishukuru kwaniaba ya wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na mji Geita, Ali Kidwaka amesema, anaushukuru Mgodi kwa kuwa msaada mkubwa kwa jamii, akiahidi kusimamia vyema ili kupata thamani ya fedha na kwamba hakika kwa sasa, wananchi wanajua mchango wa fedha hizo kutoka GGML kwani zimeigusa jamii kwa mapana zaidi.
Utiaji saini makubaliano hayo umeshuhudiwa na wajumbe wa kamati za usalama mkoa na wilaya, wenyeviti wa halmashauri hizi mbili, wakurugenzi, wanasheria kutoka sekretarieti ya mkoa na halmashauri za mji na wilaya geita, timu za CSR pamoja na waandishi wa habari.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa