Hayo yamejiri wakati wa Kikao cha Kamati Jumuishi ya Lishe Mkoa wa Geita kilichofanyika tarehe 19.01.2019 katika ofisi ya Mganga Mkuu, Mkoa wa Geita
Akiongea kabla ya kuweka kikao wazi, Mwenyekiti wa Kamati na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Geita Bw.Herman Matemu amesema kuwa, taarifa zinaonesha kuwa bado mkoa wa Geita haujafanya vizuri katika suala zima la lishe, hivyo kusema kuwa kamati inatakiwa kuwajibika kwa kushauri ipasavyo kupitia taarifa zao na mwisho wa siku watendaji kutekeleza vizuri ili kuinua asilimia ya lishe bora ndani ya mkoa.
Amesema, “kama kamati tunao wajibu wa kufanikisha suala zima la lishe kila mmoja katika kila eneo lake na kusema hata kuwa, kwenye eneo la kilimo twapaswa kuwaelimisha wananchi ili walime mazao mchanganyiko yatakayowawezesha kupata mazao yenye kuwapatia lishe iliyo bora na kusisitiza kuwa bado upo umuhimu wa kuwakutanisha wadau wanaoshughulika na lishe ndani ya mkoa, wawasilishe mipango yao ili kuepusha migongano katika utekelezaji wake bila kusahau kuwa Halmashauri zote zinatakiwa kuendelea kuweka na kutenga kwenye bajeti fedha kwaajili ya lishe.”
Katika kikao hicho, wajumbe wamekumbushwa kuhakikisha wanawasilisha mpango mkakati wa kila sekta wa namna shughuli za lishe zitakavyokuwa zikitekelezwa kwenye kikao kijacho, ambapo awali shughuli za lishe zilitekelezwa na watumishi wa afya kwa kiwango kikubwa.
Halmashauri bado zinaelekezwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya shughuili za lishe ili zisikwame wakitambua kuwa, serikali imetilia mkazo suala hilo kwamba ni muhimu sana kuzingatia, huku Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa kupitia Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Japhet Simeo ikiahidi kuwa,hadi kufikia mwezi machi, 2019 wanatarajia kuanzisha utaratibu wa kutengeneza chakula dawa japokuwa tayari wameweka kwenye bajeti ununuzi wa chakula dawa cha kisasa kupita bohari ya dawa MSD.
Nao wajumbe wakiwemo wadau wa lishe Mkoa wa Geita wameahidi kukutana wakati utakapofika ili kwa pamoja waje na mpango utakaorahisisha utekelezaji na isiwe kama awali ambapo kuna mahala wamejikuta wakitekeleza shughuli moja ilihali wadau ni tofauti
Awali afisa Afya Mkoa Bi. Tibezuka John aliwaeleza wajumbe kuwa, hadi robo ya pili yaani mwezi Oktoba hadi Desemba 2018, shughuli mbalimbali zimetekelezwa zikiwemo usimamizi na ufuatiliaji shirikishi, vikao vya kamati jumuishi vya lishe, kutembelea kaya na kutoa elimu ya ufahamu kwa lengo la kupunguza udumavu n.k
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa