Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Martine Shigela ametoa pongezi kwa Halmashauri Sita za Mkoa wa Geita ambazo ni Bukombe, Chato, Nyang’hwale, Geita Mji na Geita wilaya kwa kupata hati safi kutokana na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali ( CAG) iliyoishia mwezi Juni 2023.
Mhe. Shigela ametoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti hivi karibuni alipokuwa akizungumza katika vikao maalum vya Baraza la Madiwani vilivyofanyika katika Halmashauri hizo kwa ajili ya kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali.
Mkuu wa Mkoa wa Geita amewashauri viongozi na wataalam katika Halmashauri hizo kuweka ratiba ya vikao vya kujadili hoja za mkaguzi ili kupunguza idadi ya hoja zoezi la uhakiki linapoanza.
“Kuna baadhi ya watendaji na wakusanya mapato ambao wamejenga desturi ya kukaa na fedha mbichi ya Serikali mikononi badala ya kupeleka benki, watu wa namna hii wanatakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria na sio vinginevyo.”Aliongeza Mhe. Shigela.
Mkuu wa Mkoa wa Geita alitumia fursa hiyo kuwaasa waheshimiwa Madiwani na wataalam wa Halmashauri zote kuendelea kuimarisha upendo, umoja na mshikamano ili Halmashauri zao ziendelee kustawi vizuri.
Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakiwa katika kikao cha kujadili Taarifa ya Mdhibiti & Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Ndugu Mohamed Gombati amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Geita kwa usimamizi makini uliofanikisha Halmashauri zote za Mkoa kupata hati safi pamoja na kuzishauri Halmashauri hizo kuhakikisha wnazingatia sheria, kanuni na taratibu ili kupunguza uzalishaji wa hoja.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa