Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli azindua Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chato ambapo huduma hiyo itawapunguzia adha wananchi wa Wilaya hiyo kwani awali walikuwa wakiipata kwenye Mahakama ya Wilaya ya Biharamulo Mkoani Kagera inayopatikana umbali wa Kilomita 80 kutokea Chato.
Akifungua Jengo hilo Mheshimiwa Rais ameipongeza Mahakama kwa Ujenzi wa Mahakama nyingi Nchini, pia Wizara ya mambo ya ndani kwa kujenga Gezera Wilayani hapo kwani hayo yote yaliwatesa sana wananchi wa Chato tangia wakati wa Uhuru.
Aidha. Mhe. Rais amesema pamoja na kuajiri Mahakimu 396 na kupandisha Majaji 50 katika kipindi cha Uongozi wake, Serikali itaendelea kushughulikia Changamoto mbalimbali zinazoikabili Taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kuajiri Watumishi kadiri inavyowezekana.
Ametumia nafasi hiyo pia kuwaonya Watumishi wa Mahakama kutojihusisha na vitendo vya Rushwa katika utendaji wao na wawe waadilifu watende haki wanapowahudumia wananchi.
Wakati huo huo Mwendesha Mashtaka wa Serikali alisema katika mwendelezo wa kupunguza mrundikano wa Mahabusu Magerezani, jana amewafutia kesi Mahabusu 150 kwenye Gereza la Geita ambao walikuwa na kesi ndogo. Alieleza pia kwa sasa Nchini kuna Wafungwa elfu 12 na mahabusu elfu 17.
Jaji Mkuu wa Tanzania Prof Ibrahim Juma alifafanua kuwa Ibara ya 107 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanznia imetambua kuwa Mahakama ndio Chombo pekee cha Utoaji haki hivyo anamshukuru Mhe. Rais kwa kuwapatia Fedha za Ujenzi wa Mkahama hiyo ili kurahisisha shughuli hizo kwa wananchi.
Wakati huohuo, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameweka Jiwe la Msingi kwenye Ujenzi wa Jengo la Zimamoto na Uhokoaji lililoanza kujengwa mwezi wa Oktoba 2019 na linatarajiwa kukamilika Februari 2020 na litagharimu jumla ya Tshs Milioni 943.
Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini, kamanda Thobias Andengenye amemshukuru Mhe. Rais kwa Ujenzi wa Ofisi hizo na akafafanua kuwa Mhe Rais hivi karibuni alitoa Milioni 713 kujenga Ofisi na kituo cha Jeshi la Zimamoto Wilayani hapo. “Jeshi hili halijawahi kupata heshima hii kubwa tangu dunia ilipoundwa" alisema Kamanda Andengenye.
Mhe. Spika wa Jamhuri ya Muungano aliwasalimia wananchi wa Chato na akawapongeza kwa malezi mazuri kwa Mhe. Rais hadi amekua tegemeo (Jembe) anayekubalika Nchi nzima. “Wananchi fuateni sheria bila shuruti na Jengo hilo ndio sehemu ya Kupata haki kwa wanyonge” alisema Spika.
Mhe. Rais ameweka pia jiwe la Msingi kwenye Msikiti Mkubwa wa kisasa Wilayani Chato wenye uwezo wa kuchukua watu elfu moja kwa wakati mmoja utaogharimu zaidi ya Bilioni 1 na Milioni Mia sita za Kitanzania.
Akizungumza na wananchi Mheshimiwa Rais kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Chato amewashukuru taasisi ya Islamic foundation kwa Msaada wa Visima vinane walivyovijenga Wilayani humo na kugharimu Milioni 340 na amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kutunza miundombinu ya Mradi huo.
Aidha, Mhe Rais alimpongeza Mhe. Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa kwa Usimamizi mzuri wa Miradi ya Maji nchini hadi kufikia 71% ya upatikanaji wa Maji mwaka huu kutoka 56% mwaka 2015.
Aidha, alimpongeza Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kwa kazi kubwa anayofanya kuuletea maendeleo mkoa wa Geita na akamtaka kusimamia vizuri Ujenzi wa Vyumba 12 vya Madarasa vinavyojengwa shuleni hapo kwani vitapunguza adha ya mrundikano wa Wanafunzi kwani ina zaidi ya Wanafunzi elfu nne.
Naye Waziri wa Maji, aliushukuru ubalozi wa nchi za kiarabu kwa kufadhili mradi huo na akaeleza kuwa Chato ni miomngoni mwa Miji 28 nchini iliyo kwenye mpango wa Kuiendeleza kutoka Fedha za Mkopo wa masharti nafuu.
Mhe. Mkuu wa Mkoa alifafanua kuwa Milioni 336 zinajenga Madarasa 12, Ofisi na Matundu ya Vyoo shuleni hapo na kwamba Ujenzi unakwenda vizuri sana.
Mwenyekiti wa Islamic Foundation amesema pamoja na Ujenzi wa Visima hivyo kwa muda wa miezi mitatu, Taasisi yao inatoa huduma za Elimu, afya na Jamii kama kulea Watoto yatima.
Abdulah Al Masoud Balozi wa Nchi za falme za kiarabu Nchini alimpongeza Mhe. Rais kwa Uongozi bora wenye matokeo chanya ya Maendeleo hasa kwa Utekelezaji wa Miradi mikubwa inayolisogeza Taifa kwenye Uchumi wa Kati.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa