Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Mheshimiwa Grace Kingalame ametoa rai kwa jamii kuhakikisha wanalinda haki za watoto na kutimiza wajibu wao katika kujenga maisha ya watoto yanayoendana na mila na desturi za kiafrika.
Mhe. Kingalame ametoa rai hiyo alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa hivi karibuni katika viwanja vya Sabasaba Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale.
Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale amewakumbusha wazazi, walezi na Taasisi zisizo za Kiserikali zinazoshughulika na masuala ya haki za watoto kuwajibika kutekeleza haki tano za msingi za mtoto ambazo ni Haki ya kuishi, kuendelezwa, kulindwa, kushirikishwa na kutobaguliwa.
“Kila mwanajamii ana jukumu la kuzuia ukiukwaji wa maadili na kuwafundisha watoto kuishi katika misingi na tamaduni za kitanzania kwa lengo la kupata kizazi endelevu kitakachoepukana na mmomonyoko wa maadili katika jamii. Mila na desturi za kitanzania zinapaswa kutambuliwa na kuendelezwa kwa kuwa zina manufaa katika kulinda na kuendeleza maadili mema ya Taifa letu”. Aliongeza Mhe. Kingalame.
Mhe. Kingalame alitumia fursa hiyo pia kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ifikapo mwezi Oktoba 2025.
Katika risala iliyosomwa na watoto wameomba Serikali na jamii kwa ujumla kuendelea kutokomeza changamoto ambazo zinawakabili watoto ikiwa ni pamoja na ongezeko la watoto wanaoishi mitaani, watoto kukosa maadili na malezi bora kutoka kwa wazazi/walezi wao, utoro mashuleni unaosababishwa na ukosefu wa mahitaji ya msingi kwa watoto, vitendo vya ubakaji na ulawiti vinavyofanywa kwa watoto, mimba katika umri mdogo, baadhi ya wazazi kuozesha mabinti wenye umri mdogo na wazazi/ walezi kutotimiza mahitaji ya msingi ya watoto katika familia zao.
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka 2025 yameongozwa na Kauli mbiu isemayo “ Haki za Mtoto: Tulipotoka, Tulipo na Tuendako.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa