JAPAN YAKABIDHI MRADI WA SOKO LA SAMAKI LA KIMATAIFA KASENDA WILAYANI CHATO WENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 320
Serikali ya watu wa Japan imekabidhi mradi wa Soko la Samaki la kimataifa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Chato wenye thamani ya shilingi milioni 320 na kusaini makubaliano ya ukarabati wa barabara ya Mganza - Kasenda ili kurahisisha usafirishaji wa mazao ya ziwani.
Akizungumza baada ya kukabidhi mradi huo kwa Serikali Balozi wa Japan nchini Tanzania Mheshimiwa Yoshida Masaharu amesema mradi huo umetolewa na Serikali ya Japan kwa watu wa Tanzania ikiwa ni mwendelezo wa urafiki wa siku nyingi katika utekelezaji wa miradi ya kilimo na uvuvi. ''Mradi wa huu ulitolewa baada ya kuona soko la Kasenda liko katika hali mbaya na samaki kuharibika kwa kukosa miundombinu ya kuhifadhi ndipo Japan ikachukua hatua za haraka kwa kutoa fedha dola za kimarekani 148,146 kwa ajili ya kujenga soko na kukarabati soko la zamani''. Utekelezaji wa mradi ulianza mwaka 2017 na sasa wananchi wanaendelea kunufaika.
Awali akisoma taarifa ya mradi huo kabla ya makabidhiano mkurugenzi wa Halmashauri ya Chato Joel Hari amesema mradi unahusisha ujenzi wa ghala kubwa la kuhifadhia samaki na ukarabati wa sokola zamani.Ameeleza kuwa soko lipo chini ya Halmashauri ya Chato likiwa na wanachama 241 huku likikasimiwa kukusanya shilingi milioni 140 kwa mwaka huku likitoa huduma kwa nchi za Rwanda,Burundi, Uganda na Congo DRC.
Kwa upande mwingine Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amemshukuru balozi wa Japan nchini kwa miradi hiyo na kumwomba kuangalia na Wilaya zingine za Mkoa wa Geita ili nazo zinufaike na miradi ya namna hiyo. Aidha, ameutaka uongozi wa soko kwa kushirikiana na Halmashauri ya Chato kuhakikisha malengo yote yaliyokusudiwa kwa mradi huo yanatekelezeka na kuleta faida ili watu wote wanaofanya kazi katika soko hilo waongeze kipato kwa kuwa kazi ya Serikali ya awamu ya tano ni kujenga miundombinu bora na kuweka mazingira wezeshi ya kusaidia kuendesha biashara.Mhandisi Robert Gabriel ameahidi kuangalia namna ya kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga vibanda vya pembeni mwa soko ili kuwe na mazingira mazuri ya kufanya biashara.
Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Nishati Mheshimiwa Medard Kalemani amemshukuru Balozi Yoshida kwa kutoa miradi hiyo Wilayani Chato na kuomba pia kusaidia ujenzi wa kiwanda cha kuunganisha magari. Amewataka wananchi wa Chato na Kasenda kutumia fursa ya uwepo wa mradi huo kujenga biashara na kutoa wito kwa wenye mitaji midogo kuitunza ili ikuwe.Katika makabidhiano hayo Serikali ya Tanzania na Japan zimesaini mkataba wa ukarabati wa barabara yenye urefu wa Kilometa 1 kutoka Mganza hadi Kasenda ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa za kutoka ziwani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa