Kampuni Ya GGM Yatakiwa Kutoa Kazi Za Huduma Kwa Wakazi Wa Geita
Mkuu wa Mkoa wa Geita na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi ameutaka Uongozi wa Kampuni ya Uchimbaji wa Madini ya Geita (GGML) kutoa fursa za utoaji wa huduma katika mgodi huo kwa vikundi mbalimbali vya Ujasiriamali vilivyoko Mkoani Geita.
Agizo hilo limetolewa hivi karibuni wakati Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Geita ilipotembelea Mgodi huo kwa lengo la kukagua na kuona namna unavyoendesha shughuli zake za kila siku.
Mhandisi Robert alitaja fursa ambazo vikundi vya ujasiriamali vya Wanawake na Vijana vinavyojishughulisha na kilimo pamoja na ufugaji katika Halmashauri za Mkoa wa Geita vinaweza kuuza bidhaa zao kwa kampuni ya GGM kama vile kuuza vitoweo vya kuku, nyama ya ng'ombe, kondoo, sungura, matunda na Mchele tofauti na hivi sasa ambapo bidhaa hizo huagizwa nje ya Mkoa wa Geita.
''Ili kukuza uchumi wa wananchi na Mkoa kuna umuhimu wa Kampuni kutoa fursa kwa vikundi vyetu ili vianze kutoa huduma kwa sababu Halmashauri za Mkoa kupitia mfuko wa wanawake na vijana wako tayari kuvikopesha mitaji vikundi hivyo ili viwe na nguvu ya kutoa huduma hizo kwa kampuni''. Aliongeza Mkuu wa Mkoa.
Aidha, aliagiza kuwa fedha ya huduma ya jamii (CSR) inayotolewa na Mgodi kwa Mkoa wa Geita lazima ifahamike kwa Umma na namna inavyotumika ili kuwa na uwazi kati ya Kampuni, Serikali na jamii inayozunguka mgodi wa GGM. Pia, aliwataka viongozi wa mgodi kuwachukulia hatua za kisheria na kuwawajibisha watumishi wao watakaobainika kutumia nafasi zao kwa maslahi binafsi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa GGM Ndugu Richard Jordinson aliishukuru kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kwa Kutembelea mgodi na kujionea shughuli zinazofanyika na kuahidi kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa.
Vile vile alieleza kuwa kuwa kampuni ya GGM itaendelea kushirikiana na jamii katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Katika Ziara hiyo kamati ya Ulinzi na Usalama ilipata fursa ya kutembelea mgodi wa chini na juu pamoja na eneo la uzalishaji (Process Plant).
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa